Tarehe 21.2.2023 Dr. Mwita Mangora Mhazili Mwandamizi wa chuo kikuu Dar es salaam kutoka taasisi ya sayansi ya bahari Zanzibar, akiwa ameambatana na Afisa mazingira wa Halmashauri ya wilaya ya Kibiti ndg. Gideon Zakayo, Meneja Misitu kutoka TFS Kibiti ndugu Davis Mlowe na Frank sima kutoka TFS makao makuu wametembelea miti ya mikoko iliyopandwa mwaka 2019 kupitia mradi wa mabadiliko ya tabianchi uliokuwa unasimamiwa na ofisi ya Makamu wa Rais Idara ya Mazingira na Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti chini ya Mkandarasi mshauri Dr. Mwita Mangora kutoka taasisi ya sayansi ya bahari chuo kikuu dar es salaam.
Aidha maendeleo ya Mikoko hiyo ni mazuri kwani Mikoko iliyopandwa imekuwa vizuri na imeanza kutoa mbegu ambazo kadri zinavyoanguka mikoko mipya inaota.
“Eneo hili halikuwa na Mikoko kabisa, baada ya kuharibiwa kutokana na shughuli za kibinadamu ila kwa sasa uoto wa asili umeanza kurejea katika maeneo yaliyopandwa mikoko” alieleza Frank Sima.
Hata hivyo katika ziara hiyo Wataalamu wamewahimiza wananchi waliowakuta kwenye msitu wa hifadhi wa mikoko wasiharibu uoto wa asili uliopo katika delta ya mto Rufiji kutokana na faida zake nyingi za kimazingira na kijamii.
“ Uoto wa asili ni vizuri ukatunzwa vizuri, Ni rahisi kuutunza uoto uliopo kuliko gharama na muda wa kupanda na kuuhudumia uoto mbadala, hivyo tusipo thamini uoto asili tulionao sasa tutaingia gharama kurudishia ” Alisema Dr. Mwita
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.