Mkazi wa Kijiji Cha Mtunda A kilichopo katika Kata ya Mtunda Wilayani Kibiti ajulikanaye kwa jina la Kiday J. Lambo ni mfugaji mwenye ng’ombe aina ya Boran na Sahiwa zaidi 500, kondoo Zaidi ya 100 na Mbuzi 150 ndani ya shamba lenye hekari takribani 1000 ameamua kuwekeza katika ufugaji maarufu kama “zero grazing ” . Ufugaji huo ni suluhu ya migogoro kati wakulima na wafugaji huria ambao mara kadhaa wamelalamikiwa kulisha mifugo yao kwenye mazao ya baadhi ya wakulima katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Mbali na kujikita katika ufugaji wa kundi kubwa la ng’ombe, Bw. Lambo hufuga mifugo mingine kama vile mbuzi, kondoo,kuku,Bata n.k. katika eneo hilo.
Hata hivyo mfugaji huyo anatarajia kuleta mashine ya kisasa ya kusaga nyasi kwa ajili ya kuhifadhi chakula cha akiba cha mifugo yake Ili wakati wa kiangazi ng’ombe wasipate shida ya chakula.
Pia Bw. Lambo amesema kama wafugaji watapewa maeneo ya kudumu watatulia na kuepukana na ufugaji wa kuhamahama na endapo akipata eneo la kudumu yuko tayari kupangiwa utaratibu wa kulipa ushuru jambo ambalo litasaidia kukusanya mapato kwa urahisi na kukuza uchumi wa Halmashauri hiyo.
Akijibu swali aliloulizwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Kibiti Mohamed Mavura kuhusu mifugo kuambukizana magojwa Bwana Lambo amesisitiza kufanyika kwa kampeni ya chanjo ya Ndigana katika kipindi hiki cha kiangazi kwani ni msimu wa mifugo kuambukizana magonjwa ya mlipuko kwani wanyama wengi hufa kwa ugonjwa huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kibiti Ndg. Mohamed Mavura amempongeza mfugaji huyo kwa kutumia fursa ya ufugaji katika kukuza uchumi kwa maendeleo yake binafsi ya Wilaya yetu na Taifa kwa ujumla. Vile vile Mkurugenzi amewataka maafisa mifugo kufanya tathmimi ya mifugo yote ili kupata idadi kamili jambo ambalo litasaidia kukusanya na kuongeza mapato katika halmashauri yetu.
Pia Bw. Mavura ametoa wito kwa wafugaji wengine hasa wa kuhama hama wajifunze kutoka kwa Kiday Lambo ambaye ameonesha nia ya kutaka kufanya vizuri zaidi katika eneo hili la ufugaji.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.