Ikiwa ni mwendelezo wa ziara za kawaida za kikazi Mkurungezi Mtendaji wa wilaya ya Kibiti Mohamed Mavura amekagua miradi miwili ya maendeleo katika Kata ya Mchukwi na kata ya Mahege kunakotekelezwa miradi ya maendeleo ya Ujenzi wa zahanati wenye jumla ya sh 100,000,000.
Katika Kata ya mchukwi Mkurugenzi amekagua mradi wa zahanati ya Nyakaumbanga wenye thamani ya Tsh. 50,000,000/= kwa ufadhili wa fedha za serikali kuu na ujenzi upo hatua ya upandishaji kuta.
Vilevile ametembelea Kata ya Mahege na kukagua mradi wa zahanati ya Nyambwanda wenye thamani ya Tsh. 50,000,000/= kwa fedha za serikali kuu, ujenzi upo hatua ya kufunga rinta na kazi zinaendelea.
Aidha Mavura amewapa angalizo mafundi kuhakikisha wanajenga kwa kiwango kinachotakiwa kwani ujenzi huo utakaguliwa na muhandisi wa majengo na endapo fundi akifanya uzembe wa kujenga chini ya kiwango ajiandae kuvunja na atafidia mwenyewe kiasi cha fedha kitakachotakiwa.
Katika ziara hiyo Mkurugenzi Mavura aliambatana na Mganga Mkuu wa wilaya Elizabeth Oming’o, kaimu afisa mipango na uchumi Amina Lilanga , Afisa maendeleo ya jamii Hawa Mchomvu na Afisa Habari.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.