Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo akiwa ameambatana na Kamati ya maafa pamoja na Viongozi wa Chama amezivunja rasmi kambi zilizotengwa kwaajili ya waathirika wa mafuriko Wilayani humo. Kanali Kolombo ametekeleza jukumu hilo katika kambi ya kitumbini tarehe 21.06.2024. Kambi hiyo iliyokuwa katika Kata ya Mtunda ilikuwa ni hifadhi kuu ya waathirika wa mafuriko Wilayani Kibiti.
Uamuzi huo wa kuvunja kambi umefikiwa baada ya mvua kuisha na maeneo yaliyoathirika kuonekana kurejea katika hali yake ya kawaida.
Akifunga kambi hiyo Kanali Kolombo amewaeleza wananchi kuwa ngazi ya Wilaya imekwishapata mbegu za muda mfupi hivyo wanaporejea katika makazi yao wakalime na kupanda mbegu hizo ili waweze kujiandalia chakula cha baadaye.
"Mliomba mbegu, tumekwishazipata, mtagawiwa katika Vitongoji mnavyotoka orodha yenu tunayo, mkapande mbegu hizo" Alisema Kolombo.
Mbali na upatikanaji wa mbegu amewaondoa hofu wananchi hao kwa kuwahakikishia kuendelea kuishi salama waendako kama walivyokuwa wameimarishiwa ulinzi kambini hapo.
Vilevile Kanali Kolombo ametoa shukrani zake za dhati kwa Mhe. Rais SSH kwa misaada aliyotoa, wadau mbalimbali, viongozi wa ndani na nje ya Wilaya kwa namna walivyojitoa kuhakikisha familia hizo zinakuwa salama.
Kuhusu maombi ya wananchi hao kupata makazi ya kudumu Mratibu wa Kamati ya maafa Wilaya ya Kibiti Ndg. Zakayo Gideon ametoa rai kwa wananchi kuridhia kwenda katika maeneo watakayogawiwa kwani mpaka sasa wamekwishapata maeneo katika Kata ya mahege ambayo ni Tomoni na Nyakinyo wakati wakisubiri maeneo mengine.
Hata hivyo katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Kibiti Ndg. Maliki Magimba akitoa Salamu za Mwenyekiti wa Chama na Mhe. Mbunge amewataka wananchi hao kushukuru Mungu kwa kila jambo na kuganga yajayo. Badala ya kukumbuka yaliyopita basi wachangamkie kilimo kwani tayari mbegu zimewasili.
Nao Wananchi waliopata hifadhi kambini hapo wameishukuru Serikali na Uongozi wote kwa namna walivyowapokea na kuwahudumia kwa kila hali ikiwemo kuimarishiwa ulinzi.
Aidha kabla ya kuondoka Kambini hapo wameiomba Serikali kuendelea kuwaimarishia ulinzi hususani katika mashamba yao kutokana na changamoto ya Mifugo, waliomba kupewa maeneo ya makazi ya kudumu na kuhakikisha mbegu hizo zinagawiwa katika Vitongoji vyote.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.