Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amefunga rasmi mafunzo ya Awali ya mgambo kundi la 8 , Jaribu mpakani katika Kata ya Mjawa yaliyoanza mwezi Julai na kuhitimishwa Leo Novemba 29 mwaka 2024.
Katika hafla hiyo jumla ya wahitimu 69 kati ya 92 walianza wamehitimu ambapo wanawake ni 11 na wanaume ni 58.
Akitoa pongezi kwa Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kuridhia mafunzo hayo Kanali Kolombo amewapongeza pia Wahitimu wote waliofanikiwa kuhitimu mafunzo hayo kwa kujitolea sambamba na wakufunzi kwa kazi nzuri ya kuhakikisha wameiva kisawasawa.
Vilevile Kanali Kolombo amewaagiza Wahitimu hao kwenda kufanya kazi kwa uadilivu kwani thamani ya Ulinzi wa wananchi ni wananchi wenyewe ikijumlishwa na Wahitimu hao.
Kwa upande wa changamoto zilizotokea wakati wa mafunzo Kanali Kolombo amewaagiza Wakufunzi kuwa na mawasiliano ya karibu na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ili kero iliyopo iweze kutatuliwa kwa wakati kulingana na ukubwa wa tatizo huku akiahidi kutafuta ufumbuzi wa haraka.
Aidha Mshauri wa Mgambo wa Wilaya Meja. Spatiel Matonya katika taarifa yake amesema wanafunzi wanaohitimu kupitia Jopo la wakufunzi wake, wamepimwa kupitia mafunzo mbalimbali kwa masomo ya darasani na ya nje kwa vitendo na kukubalika.
Awali katika risala ya Wahitimu iliyosomwa kwa Mgeni rasmi ilieleza changamoto mbalimbali wanazopitia na kuomba Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kuwasaidia kugharamia sare ya mafunzo, buti , chakula cha Wakufunzi na Wanafunzi , kulipiwa vyeti na vitambulisho huku wakisisitiza kupewa kipaumbele cha kujiunga na jeshi la Kujenga Taifa nafasi zinapotokea.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.