Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Mhe.Kanali Joseph Kolombo amepokea Taarifa ya zoezi la uandikishaji Kaya kwaajili ya Kampeni ya ugawaji Vyandarua katika kila Kaya lengo ikiwa ni kuongeza umiliki wa vyandarua kufikia asilimia 80 katika jamii.
Afua hii ya matumizi ya vyandarua,inayolenga kutokomeza ugonjwa wa Malaria imeonyesha ufanisi wa asilimia sitini ikilinganishwa na afua nyingine zinazo tekelezwa zikilenga pia kutokomeza ugonjwa huu wa Malaria.Kampeni hii inaenda sanjari na utoaji vyandarua katika jamii kupitia Watoto chini ya miaka mitano,akina mama wajawazito na makundi maalumu.
Akizungumza wakati wa kupokea Taarifa hiyo ya zoezi la uandikishaji Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Mhe.Kanali Joseph Kolombo amewataka wanachi wa Wilaya ya Kibiti kuwa na matumizi sahihi ya vyandarua hivyo pindi vitakapowafikia ili kuendana na matakwa ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye lengo la kutokomeza ugonjwa wa Malaria ifikapo mwaka 2030.
Aidha ametoa rai kwa Wataalamu wa Afya na wajumbe wanaounda timu ya Wilaya ya uratibu wa zoezi hilo kuhakikisha wanafanya kazi kwa ufanisi ili kufanikisha zoezi la ugawaji wa vyandarua kama ilivyokusudiwa.
Kampeni hii ni mojawapo ya Afua muhimu kuelekea lengo la kutokomeza Malaria na inaratibiwa na Wizara ya Afya, OR-TAMISEMI, Bohari kuu ya Dawa (MSD) na Mfuko wa Dunia wa kupambana na magonjwa ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund)
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.