Afisa Tarafa wa Tarafa ya Kibiti Ndugu Salim Mzaganya leo Juni 30,2025 amezindua rasmi Zoezi la Utekelezaji wa Kampeni ya Taifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo Kitaifa katika Wilaya ya Kibiti yenye lengo la kuhakikisha usalama wa mifugo, kuimarisha uzalishaji wa mifugo nchini, na kukuza pato la mfugaji kwa kupunguza vifo vinavyosababishwa na magonjwa hatari ya mifugo.
Ndugu Mzanganya amezindua kampeni hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo ambapo katika uzinduzi huo amewaasa wataalamu kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii na weledi ili kuhakikisha wanafikia malengo kama ilivyokusudiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha Mzaganya ametoa wito kwa wafugaji wote wa Wilaya ya Kibiti kushiriki kikamilifu na kuwapa ushirikiano wataalamu waliopo katika timu hizo ili kupata huduma bora na zenye tija katika kuendeleza mifugo yao.
Awali Afisa Mifugo wa Wilaya Ndugu Boniface Yohana alieleza kuwa katika kipibindi chote cha uendeshaji wa kampeni hii, Wataalamu katika Wilaya ya Kibiti wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wanawafikia wafugaji wote kwa wakati kama ilivyokusudiwa.
Hata hivyo Uzinduzi huo ambao umeenda sambamba na mafunzo ya mtandao ya uingizaji taarifa za utekelezaji wa kazi hiyo kwa wataalamu.
Takribani Kuku 1,610 Wamechanjwa hii leo katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kibiti ambapo kwa mwaka huu wa utekelezaji wa awamu ya kwanza ya kampeni Halmashauri imelenga Kuchanja kuku 130,000 ng’ombe 43,000 na mbuzi 32,000
Kampeni hii ya miaka mitano ilizinduliwa tarehe 16 Juni, 2025 katika Mkoa wa Simiyu na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.