Mtoto wa miaka kumi na mbili ( 12) Mkazi wa kibiti kusini aliyejulikana kwa jina la Ibrahim Mohamed Kakatu, mwanafunzi wa darasa la 6 katika shule ya msingi Kibiti amepatikana akiwa amefariki katika eneo la Mtawanya A kitongoji cha Umikendo Kata ya Mtawanya Wilaya ya Kibiti baada ya kupotea tangia tarehe 12 mwezi Novemba mwaka huu akiwa anacheza na wenzake.
Jeshi la Polisi Wilaya ya Kibiti lilifika eneo la tukio ambapo mwili wa marehemu umepatikana katika Kijiji cha Mtawanya A, baada ya taarifa kutolewa na msamaria mwema aliyeuona mwili huo jina limehifadhiwa kwa usalama zaidi na uchunguzi unaendelea.
Kwa mujibu wa Daktari Mashauri Matiku wa kituo cha afya cha Kibiti ambaye alifika eneo la tukio kufanya uchunguzi wa kitaalam kutambua chanzo cha kifo hicho amesema ni vigumu kutambua kwani mwili ulikwisha haribika.
Kwa mujibu wa taarifa za awali mpaka siku marehemu Ibrahimu anapotea alikua akicheza na wenzake ndipo akatokea mtu asiyejulikana na kuuliza kati yao ni nani anaejua kuendesha baiskeli? Ndipo marehemu alijibu kuwa anajua hivyo mtu huyo akampa sh. 3000 na kumwagiza kwenda kumkodishia baiskeli matokeo yake Ibrahimu hakurudi mpaka mwili wake kupatikana akiwa amefariki.
Aidha, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Meja Edward Gowele akiambatana na viongozi wa ulinzi na usalama wameshiriki katika zoezi la kuhifadhi mwili wa marehemu Ibrahimu na akiwa hapo Mhe. Gowele amesikitishwa nakulaani vikali mauaji ya kijana huyo, vilevile ameagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuchunguza na kuhakikisha waliohusika na mauaji wanapatikana na kuchukuliwa hatua za kisheria. Vilevile ameagiza nakusisitiza kwa wamiliki wote wa mashamba pori waliotelekeza maeneo yao bila kulima wala kusafishwa wahakikishe yanakuwa wazi muda wote kuanzia sasa kwa ajili ya usalama na pia amewataka wananchi kuachana na Imani potofu ikiwemo Ushirikina kwani zinachangia sana vitendo hivyo viovu.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.