Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Ndg. Hanan Bafagih amekutana na Wakuu wa Shule za Sekondari Wilayani humo kwa lengo la kufahamiana na kusikiliza kero mbalimbali wanazokutana nazo katika majukumu yao ya kila siku.
Awali Wakuu hao wa shule kwa nyakati tofauti wakitoa kero zao wamesema changamoto zinazowakabili ni pamoja na kutololipwa stahiki za uhamisho na likizo kwa wakati, mifumo ya utekelezaji wa miradi kuchelewa, utoro wa wanafunzi, upungufu wa walimu, jamii kutokuwa na utayari wa watoto wao kusoma, uhaba wa samani, umeme na maji kwa baadhi ya shule.
Mara baada ya kusikiliza kero za wakuu hao wa shule, Mkurugenzi Bafagih ameziagiza idara ya Utumishi na Elimu kumshirikisha katika kila jambo kabla ya kuchukua maamuzi yeyote huku akisisitiza kuwa, madai yao yatatekelezwa kwa wakati.
Vilevile Ndg. Bafagih amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa upendo, kujiamini, kuheshimiana, kushirikiana na kuvumiliana katika utendaji sambamba na kuwa na subira katika majambo yao wakati yanafanyiwa kazi.
" Naomba muwe na uvumilivu kwa changamoto yeyote Ofisi yangu iko wazi , ikiwezekana tengenezeni utaratibu wa kuwasilisha changamoto zenu kwangu moja kwa moja jumbe zote nitasoma" Alisema.
Aidha akijibu changamoto zilizoainishwa na Walimu kaimu Afisa Elimu Mwl. Shabani Mangosongo amewatoa hofu walimu akisema Serikali ipo kazini na kila mmoja atapata stahiki yake. Pia kupitia kikao hicho amewataka walimu kujitathamini wenyewe kwenye majukumu yao.
Kwa niaba ya Walimu, Makamu Mwenyekiti TAHOSA, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Kibiti Mwl. Lawrence Mwakyoma amemshukuru Mkurugenzi kwa kutenga muda wake na kusikiliza kero za walimu. Hata hivyo ameahidi kuwa wanakwenda kufanya kazi na kuwa viongozi wa mfano.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.