Ni katika ukumbi wa mikutano uliopo ndani ya jingo la Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti limefanyika Baraza la madiwani mahususi kwa ajili ya kujadili majibu ya hoja za ukaguzi kama zilivyo ainishwa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG). Baraza hilo liliongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Ramadhani Mpendu na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge, Mkuu wa Wilaya Mhe. Kanali Joseph Kolombo, Mkaguzi Mkazi wa Mkoa wa Pwani (Chief External Auditor) Mary Dibago, Wahe. Madiwani, viongozi wa chama cha Mapinduzi, Wakuu wa idara/vitengo n.k
Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri Ndg. Denis Kitali ambaye ndiye Katibu wa Baraza hilo alitoa taarifa fupi juu ya hoja zinazoikabili Halmashauri hiyo, ambapo alieleza kuwa katika ukaguzi wa 2021/2022 Halmashauri ilitunukiwa hati safi ikiwa na jumla ya hoja 49, kati ya hizo 18 zimefungwa na 31 bado hazijafungwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kufuatilia vielelezo mbalimbali ili kuzifunga hoja hizo. Pia kulikuwa na hoja 15 za miaka ya nyuma ambapo 10 zimefungwa na 05 zinaendelea. Hivyo hoja zote zilizobaki zitahakikiwa upya katika ukaguzi ujao.
Kufuatia mjadala huo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani ametoa maelekezo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti kuchambua na kutoa hoja zote ambazo ziko nje ya uwezo wa Halmashauri kiutendaji na kuziwasilisha kwa Katibu Tawala wa Mkoa ili ziweze kuwasilishwa kwake Mhe. Rais.
" Mkurugenzi Mtendaji nakuagiza chambuweni kesi zote za muda mrefu zenye maslahi ya Serikali na kuziwasilisha kwa Katibu Tawala wa Mkoa." Alisema Kunenge.
Kunenge amewaagiza wasimamizi wa miradi kusimamia miradi yote vizuri na kuhakikisha inakamilika kwa wakati bila kusahau miradi iendane na thamani ya fedha iliyopangwa. Kwani itakuwa ni jambo la aibu ikiwa fedha za miradi husika zitashindwa kumaliza mradi uliopangwa.
"Hii haikubaliki kabisa, fedha inatolewa taslim, miradi haikamiliki, lazma tujiulize fedha zinakwenda wapi? " Alisema Kunenge.
Kunenge akizungumzia umuhimu na utunzaji wa nyaraka amesema suala la ukaguzi ni utaratibu endelevu na wa kawaida kabisa nchini kila mwaka, mjipange kuandaa nyaraka amapema kabla ya ukaguzi.
Hata hivyo kupitia Taarifa iliyowasilishwa wa Mkaguzi wa ndani wa Wilaya ndg Richard Mwalonda, Mkuu wa Mkoa Kunenge ameagiza kufanya kazi kwa kufuata ushauri wa Mkaguzi huyo ili kuweza kufanya kazi kwa weledi.
Aidha Kunenge ameagiza kuwepo kwa usimamizi mzuri wa mapato katika Halmashauri ili kuweza kupata mapato mengi na kumsaidia Mhe.Rais kuweza kutatua changamoto zinazowakabili wananchi kwa wakati huku akisisitiza kuwa Rais anahitaji kuona mchango wa pato la Taifa Kila mwaka .
Licha ya Kibiti kuwa na hati safi Mhe. Kunenge amewaagiza wakaguzi kuhakikisha wanaandaa hesabu zao kwa kufuata utaratibu ili ikawe hati yenye tija, kwa kuweka mipango yenye vipaumbele sahihI.
Katika mkutano huo Mkaguzi Mkuu wa nje wa Mkoa wa Pwani Bi Mary Dibago amewaagiza Madiwani na Wataalam kuhakikisha hoja zote ambazo hazijajibiwa zinajibiwa.Pia Bi Mary amewaagiza wataalam kuhakikisha wanasimamia vizuri miradi yote hasa katika ngazi za chini kama zahanati, vituo vya afya, hospitali au shule kwani ndiko zinakozaliwa hoja nyingi.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya kibiti Mhe. Ramadhan Mpendu,akihitimisha baraza hilo, amemsihi Mkuu wa Mkoa kusaidia upatikanaji wa banio ambalo litakuwa suluhisho la kilimo na ni UTI wa mgongo wa mapato ya Wilaya ya Kibiti.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.