Baraza la Madiwani Wilayani Kibiti limekutana katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo tarehe 15.2.2024 kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa Miradi mbalimbali kwa robo ya pili ya Mwaka wa fedha 2023/2024 na wote kwa pamoja wameridhia na kuzipitisha taarifa hizo.
Akitoa salamu za serikali Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amelishukuru baraza la Madiwani kwa mshikikamano na kuwataka kuendelea kudumisha ushirikiano kuhakikisha kibiti inasonga mbele.
Kanali Joseph Kolombo amesema hali ya Usalama wa wananchi wa Kibiti ni shwari, kwa upande mazao amewataka wananchi wa Kibiti kuanza tabia ya kulima kwa kutumia mbolea ili kuweza kupata mazao ya kutosha, ambapo kwa msimu uliopita wameweza kuvuna Tani 39 za mahindi kati ya 49 ambayo walikuwa wamejikadiria.
Kwa upande wa Elimu manjenzi yanaendelea vizuri katika hatua mbalimbali na tayari wamekwisha kamilisha agizo la Tamisemi Ujenzi wa shule ya Sekondari Chief Hangaya, Shule ya Msingi Itonga n.k zimekamilika na wanafunzi wameanza kusoma. Pia Kolombo amesema kwa msisitizo kuwa suala kuongeza jitihada za ufaulu kwa wanafunzi Mkoa wa Pwani likawe ni ajenda kuu kuhakikisha Ilani ya Chama Tawala inatekelezwa.
"Shule zipo na zinatoa huduma naomba tushirikiane kuhamasisha watoto kuripoti shuleni, mpaka sasa mahudhurio kwa shule za Sekondari ni 89% , shule ya Msingi kwa darasa la kwanza ni 46% madarasa ya Awali ni 60%. Tumefikia viwango hivi kwa jitihada kubwa, hapo sio mwisho tuendelee kupambana ufikie 100%" Alisema Kolombo.
Vilevile kwa upande wa Idara ya Afya amesema Wilaya imepokea fedha kwa ajili ya vifaa tiba na majenzi mbalimbali ambayo yanaendelea vizuri katika kituo cha Afya nyamatanga, ngondae na mbawa, wakati miradi mitano ya maji iko katika majaribio.
Salamu nyingine za Serikali ambazo alileta Kanali Kolombo ni kuongeza uzalishaji wa zao la korosho, kwakuwa zao hilo ni Uti wa mgongo wa mapato Wilayani ya Kibiti, sambamba na kuongeza jitihada za kukusanya mapato ya Halmashauri ili kuweza kumudu changamoto za Wananchi wa Kibiti.
Pia Mkuu huyo wa Wilaya ameelekeza wananchi wa Kibiti kupitia Baraza Hilo kuhimizana kuhakikisha watoto wenye umri unaoanzia miezi 9 mpaka wenye umri chini ya miaka mitano kupelekwa kupatiwa chanjo ya Surua na Rubella hata kama wamekwisha chanjwa awali. Chanjo hiyo itatolewa kuanzia tarehe 15 - 18 mwezi huu katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kibiti.
Baraza hilo pia limeridhia na kupitisha Mpango wa Bajeti ya Tsh. Billion 27,577,630,256.00 kwaajili ya mwaka wa fedha 2024/2025. Fedha hizo zitatumika kutekeleza shughuli mbalimbali za utoaji huduma, utawala na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Akiwasilisha rasimu ya Mpango na Bajeti ya mwaka 2024/2025 kwaniaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Afisa Mipango na Uratibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Bw. Ponsian Kazee ameeleza kuwa bajeti hiyo imezingatia miongozo ya kitaifa na halmashauri. Miongozo hiyo ni pamoja na kupokea mapendekezo kutoka kwa wajumbe mbalimbali kutoka katika ngazi ya Wilaya, Kata, Vijiji, Vitengo na Divisheni za Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti.
Aidha, Bw. Kazee amefafanua kwamba katika rasimu hiyo ya Bajeti , kiasi cha shilingi 15,775,015,600.00 ni kwaajili ya mishahara ya Watumishi, kiasi cha shilingi 3,529,748,056.00 kwaajili ya matumizi mengineyo na kiasi cha shilingi 8,240,873,800.00 ni kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Maendeleo.
Vilevile Baraza hilo lilipata wasaa wa kumpongeza Kijana Azizi Hassan Mlanzi wa Shule ya Sekondari Mjawa baada ya Kufanya vizuri kwenye mitihani yake ya kidato cha nne 2023. Mwanafunzi huyo alipata ufaulu wa Daraja la kwanza la pointi 7 (Div I - 7).
Madiwani hao pia walitoa Pongezi nyingi kwa Afisa Elimu Sekondari wilayani Kibiti Mwl. Anna Shitindi, walimu wa Kijana huyo pamoja na walimu wengine wote kwa jitihada zao za kuwaelimisha watoto wa Kibiti. Hii ni mara ya kwanza kwenye historia ya Elimu Wilayani Kibiti kupata ufaulu wa namna hii kutoka kwenye shule za Kata.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kibiti Mhe. Ramadhan Mpendu akifunga kikao hicho amesema wameipitia bajeti na kuipitisha wakiwa na Imani na Wataalamu kuwa wamefanyia Kazi vipaumbele vyote kama ilivyo kwenye mwongozo wa uandaaji bajeti lakini pia maelekezo na maagizo yote waliyopewa katika kikao hicho wameyapokea na watayafanyia kazi.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.