16.08.2024
Mwenyekiti wa Baraza la Wahe. Madiwani wa Halmshauri ya Wilaya ya Kibiti Mhe. Ramadhan Mpendu amewataka wakazi wa kibiti kutumia vizuri msimu huu wa korosho kupulizia mashamba yao kwa umakini kwa kutumia pembejeo za ruzuku ambazo Mhe. Rais amezitoa sambamba na kuendelea kuitunza mikorosho hiyo ambayo ni moja ya zao la kiuchumi Wilayani humo.
Pamoja na changamoto ya mvua za msimu uliopita kuathiri mikorosho amewasisitiza wakulima kupitia na kukagua mashamba yao na kuwajulisha maafisa ugani endapo kuna shida huku akimsihi Mkurugenzi Mtendaji kusimamia suala hilo kupitia wataalam wake.
Mhe. Mpendu amesema hayo alipokuwa akifungua mkutano wa BARAZA la Wahe. Madiwani uliofanyika August 15, 2024 katika ukumbi wa Halmashauri hiyo, kwa lengo la kujadili na kupokea taarifa mbalimbali za robo ya 4 kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Mbali na kupokea taarifa kwa upande wa masuala ya kiutumishi Baraza limeridhia shauri la Mtumishi mmoja ambaye ni Afisa Elimu Kata ya Mchukwi Mwl. Martine Peter Benjamin kukatwa mshahara kwa 15% kwa muda wa miaka 3 kwa utovu wa nidhamu, kutokana na utoro wa kutofika ofisini kwa zaidi ya siku 5.
Uamuzi huo umepitishwa baada ya mhusika kukutwa na hatia kupitia kanuni ya 42 (1) ambacho adhabu yake ni kufukuzwa kazi, kushushwa cheo na kupunguziwa mshahara au kukatwa mshahara kwa 15% kwa muda wa miaka 3 mfululizo. Hivyo baraza limewataka Watumishi wote kutii sheria kwa kadri inavyotakiwa kwani maamuzi kama haya huwa hayafurahishi.
Kwa upande mwingine Baraza limepongeza na kutoa ushauri kwa Taasisi za TARURA, RUWASA na TANESCO kwa jitihada zao za kufikisha huduma kwa jamii huku wakisisitiza huduma hizo zifike maeneo yote kwa wakati.
Mara baada ya ufunguzi Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo alitoa Salam za Serikali akisema Kibiti ni salama changamoto iliyokuwepo ya wakulima na wafugaji tayari wameshaanza oparesheni ya kutatua mgogoro huo.
Katika kutatua changamoto hiyo Kanali Kolombo ameliomba Baraza la Madiwani kuridhia utoaji wa hati za kimila kwa wafugaji waliotambuliwa ili waweze kuendeleza vitalu watakavyogawiwa.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya aliainisha kuwa, mpaka sasa tayari vitalu 107 vimeshapimwa kati ya hivyo vitalu 10 ni vya Kijiji cha Uchembe na vilivyosalia ni vya Mtunda na Muyuyu tayari kwa kutekeleza agizo la Mhe. Rais SSH la kuanzisha Ranchi ndogo.
Aidha kutokana na uchache wa mavuno ya mazao ya chakula, Mkuu wa Wilaya aliwasihi Waheshimiwa Madiwani kuwasisitiza wananchi kulima mazao ya chakula zaidi ili Wilaya iweze kuzalisha na kuwa na chakula cha kutosha.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.