Mkuu wa wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo ametoa rai kwa Waheshimiwa Madiwani kuhimiza wananchi kujitokeza kuchukua mkopo wa 10% kwani Bado ngazi ya Wilaya vikundi ni vichache ukilinganisha na fedha iliyotolewa sambamba na kutoa elimu ya kwa kushirikiana na Idara ya Divisheni ya maendeleo ya jamii.
Vilevile amesema Kuna haja ya kuimarisha ulinzi wa miundombinu mbalimbali inayohujumiwa na baadhi ya wananchi wasiowaaminifu ili ikaweze kutumika vizuri na kwa muda mrefu kwenye jamii husika pamoja na kulipa bili kutokana na matumizi yao hususani kwenye maji.
Kanali Kolombo amesema hayo alipokuwa akitoa Salamu za Wilaya ya Kibiti katika Baraza la Waheshimiwa Madiwani lililoketi Novemba 22, 2024 kujadili taarifa mbalimbali kwa mwaka wa Fedha 2024/2025 robo ya kwanza.
Kwa upande wa taarifa ya TARURA Mkuu huyo wa Wilaya ameshauri bajeti inapotolewa nguvu kubwa ielekezwe kutengeneza maeneo korofi ili kurahisisha kuweza kupitika kwa urahisi zaidi kwa mwaka mzima.
Mbali na hayo Kanali Kolombo amethibitisha kuwa hali ya Ulinzi na usalama wa raia ni salama huku akisisitiza wananchi wote kujitokeza kwa wingi kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika jumatano ya wiki ijayo ya Novemba 27 mwaka huu.
Hata hivyo taarifa zilizojadiliwa katika baraza hilo ni taarifa za miradi wa WDC kutoka katika Kata zote 16, taarifa za Kamati za kifedha ( Kamati ya uchumi, fedha, Ujenzi na mazingira, huduma za jamii, maadili na Kamati ya ukimwi na Taasisi mbalimbali za TARURA, RUWASA na TANESCO na kupokekelewa na Baraza hilo.
Aidha Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Ndg.Denis Kitali katika mkutano huo amesema ngazi ya Wilaya maelekezo maoni na ushauri wamepokea na watayafanyia kazi.
Akifunga mkutano huo Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe. Ramadhan Mpendu amewashukuru Waheshimiwa madiwani ,Wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na Wataalam kwa michango yao na kushiriki hususani katika msiba wa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Marehemu Mhe. Omari Twanga, aliyefariki Dunia Novemba 19 na kuzikwa November 20 mwaka huu.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.