Baraza maaluum la Wahe. Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti limeketi tarehe 30.08.2024 ili kupitia na kuridhia hesabu za Halmashauri hiyo za kufunga mwaka wa fedha 2023/2024.
Wajumbe wote kwa pamoja wameridhia hesabu hizo kama zilivyoandaliwa na kuwasilishwa na Mweka Hazina wa Halmashauri hiyo Ndg. Theonest Kibuga, kwani hazikuonekana kuwa na dosari yeyote.
Akizungumza kwaniaba ya Mkuu wa Wilaya, Katibu Tawala Wilaya ya Kibiti Bi. Maria Katemana aliwapongeza Wajumbe kwa kikao kizuri, kazi wanazofanya pamoja na kuridhia taarifa iliyowasilishwa kwenye kikao hicho, huku akitoa pongezi nyingi zaidi Wataalam kwa kazi kubwa waliyofanya ya uandaaji hesabu hizo kisha akatoa maagizo ya Mkuu wa Wilaya:
“Mkuu wa Wilaya ameniagiza niwaambie kama tulivyoona kuna tahadhari zimetolewa na mamlaka ya hali ya hewa nchini kuwa mvua za mwaka huu zinaweza kuwa za wastani au chini ya wastani basi tuhimize sana wakulima watumie vizuri mazao ya chakula waliyo nayo na pia walime yale mazao ambayo yanastawi kwa muda mfupi na yale yanayostahimili ukame”.
“Mhe. DC ameagiza pia wakulima wa mbaazi ambao tayari wamekwishaanza kuvuna wasiuze zao hilo kiholela, wahakikishe zao hilo linauzwa kwa utaratibu kama mazao mengine kwa kupeleka kwenye vyama vyao vya msingi kisha kupelekwa katika ghala kuu kwaajili ya kufanyiwa mnada kama ilivyoagizwa na Serikali” Alisema Bi. Katemana.
Aidha Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibiti Mhe. Juma Ndaruke akahitimisha kuchangia hoja kwenye kikao hicho kwa kutoa pongezi nyingi kwa Wahe. Madiwani pamoja na Wataalam kwa maandalizi na mjadala mzuri.
“Kipekee nikupongeze Mhe. Mwenyekiti wa baraza pamoja na Madiwani wako bila kuwasahau Wataalam wetu kwani namna ambavyo taarifa hii imeandaliwa na kuwasilishwa inadhihirisha wazi kabisa kuwa kazi nzuri imefanyika katika Wilaya yetu. Sisi kama chama tutaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Serikali yetu kuhakikisha kwamba lile ambalo tumewagiza mnaenda kulitekeleza katika maeneo mbalimbali na kuturahisishia uchaguzi huko tunakoenda” Alisema Mhe. Ndaruke.
Mwisho, Mwenyekiti wa baraza la hilo Mhe. Ramadhani Mpendu akafunga kikao hicho kwa kuwataka Wahe. Madiwani, Mkurugenzi pamoja na Wataalam kutobweteka na pongezi zilizotolewa kwao, badala yake waendelee kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha kila kitu kipo kwenye utaratibu wake ili miaka ijayo mambo yawe vizuri zaidi.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.