Benki Kuu ya Tanzania (BOT) tawi la Dar es Salaam imetoa mafunzo kwa watumishi wa umma na wafanyabiashara wa Wilaya ya kibiti juu ya utunzaji bora wa fedha na namna ya kutambua alama zilizopo ikiwa ni utaratibu wa kawaida nchini kadri bajeti itakavyoruhusu ambapo wameanza na Mkoa wa Pwani.
Akitoa Elimu kwa nyakati tofauti katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri na stendi kuu ya mabasi Kibiti, Mkuu wa msafara Restituta Minja kitengo cha sarafu amesema ,fedha zinatakiwa kuhifadhiwa katika bahasha au pochi ili kuepuka zisijikunje na kuchanika kwani uchakavu wa fedha huisababishia serikali hasara kubwa kwa sababu fedha mbovu zote huchambuliwa na kuharibiwa.
Vilevile Minja amesisitiza kuwa fedha zihifadhiwe katika maeneo safi na makavu na ili zisijikunje ni muhimu kuwa na pochi (wallet) imara au kasha la kuhifadhia ,sarafu na noti pia sambamba na kuzihifadhi katika maeneo yasiyo na vumbi kemikali au vyombo vinavyotoa rangi ambapo si rahisi moto,maji ,wadudu na wanyama kufikika kwa urahisi kwani fedha kwa asilimia 100 hutengenezwa na pamba na ni rahisi kuharibika au kuteketea.
Hata hivyo amekemea utunzaji mbaya wa fedha kama vile kufinyanga noti au kuikunja mkononi,kuweka noti au sarafu kwenye soksi au chini ya godoro,kuweka fedha kwenye uchafu na unyevunyevu,kuhifadhi fedha kwenye nguo za ndani au kufunga katika pindo ya kitenge au kanga hasa kina Mama ambao pia huifadhi kwenye maziwa na kuchimbia noti au sarafu aridhini utunzaji huo haustahili kutumia .
Katika hatua nyingine Minja amesema kila mwananchi anajukumu la kujua alama za fedha ili aweze kuzitambua panapotokea changamoto ya fedha feki na utapeli huku akisisitiza wafanyabiashara kuepuka kupokea fedha taslimu kwani ni chanzo cha kupokea fedha feki kwa kuchanganywa na fedha salama na halali.
Alama za kiusalama kwenye fedha hutambulika kwa njia tatu ambazo ni kwa njia ya macho kwa kusaidiwa na mwanga,kwa njia ya kuhisia na kwa njia ya tochi maalum ambayo ni kifaa maalum (uv tortch.)hususani katika eneo lenye giza huonyesha baadhi ya alama zilizojificha .
Aidha Mwezeshaji Minja amesema Tanzania haina kiwanda cha kutengeneza fedha hivyo zoezi hilo hukamilika kwa kutoa zabuni,nje ya nchi ,na ufanyika kwa ushirikiano na usiri mkubwa.Pia benki kuu imeunda sera ambayo itamwezesha mtanzania yeyote kufika benki iliyo karibu kubadilishiwa fedha zilizochakaa kwa utaratibu maalum Kwa maelekezo kutoka BOT ikiwa ni pamoja na sarafu zilizochakaa.
“Kutokana na uwepo wa alama mbalimbali kwenye fedha,ifike wakati serikali iwe na mzabuni mmoja wa kutengeneza pesa hizo ili kuepuka kuwa na alama nyingi”alisema mfanyabiashara aliyewakilisha wananchi wa kibiti
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya na watumishi wa umma Katibu Tawala wa Wilaya Milongo Sanga ameipongeza Benki Kuu kwa kutoa mafunzo ya Elimu ya uhifadhi na utambuzi wa fedha,na anaimani kubwa wananchi na watumishi wameelewa pia ametoa wito kwenye mabenki kusitisha kutoa fedha zilizochakaa na elimu hiyo kuwa endelevu.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Mohamed Mavura alitambulisha ugeni kutoka benki Kuu na kuwataka watumishi kusikiliza kwa makini kwani mafunzo hayo ni ya muhimu katika maisha ya kila siku.
Mara baada ya Mafunzo kukamilika Afisa Biashara wa Wilaya Sadelick Kihongosi ameishukuru Benki Kuu kwa kutoa mafunzo,mbali na kuwafundisha watumishi wa umma na wafanyabiashara Elimu ya utambuzi na uhifadhi bora wa fedha ni muhimu kwa wananchi wote kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu .
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.