Shirika lisilo la kiserikali la CAMFED linalotekeleza majukumu yake katika Wilaya 5 za Mkoa wa Pwani limetoa mafunzo ya siku 5 kwa wasichana wajasiliamali wa Wilaya za Kibiti, Chalinze, Bagamoyo, Rufiji na Kibaha kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kibiashara ili waweze kujisimamia na kujikwamua kiuchumi. Shirika hili linajishughulisha na kusaidia watoto wa kike katika masuala ya elimu na kuwawezesha kiuchumi ili waweze kujitegemea sambamba na kujikwamua kwenye wimbi la umasikini kwa ujumla.
Akifunga mafunzo hayo Afisa Elimu kata wa kata ya umwe bi Lucy Kisonga amewataka washiriki hao kutumia vizuri mafunzo waliyopata ili yakalete tija kwa baadae katika kuhakikisha wanajiwezesha wenyewe.
“mafunzo mliyopata Leo ni muhimu Sana yatumieni katika mtazamo chanya, sehemu nyingine washiriki huyapata kwa kulipia pesa nyie mmepewa bure, katimizeni malengo ya ndoto zenu” alisema Mwl.Kisonga.
Vilevile amewataka washiriki hao kutumia fursa hiyo kujipandisha thamani kwani wasichana wengi wameharibikiwa na mara nyingi huingia katika vishawishi kutokana na kutokuwa na kitu chochote cha kufanya na kujiingizia kipato.
“msidharau mafunzo haya ni bahati mmepata,maarifa haya mkayatumie na kuwafikishia wenzenu ambao hawajabahatika kupata nafasi hii” alisema Mwl.Kusonga.
Aidha Mratibu wa mradi wa CAMFED Wilaya ya Kibiti Bi. Shida Athman amesema wamefanikiwa kutoa mafunzo kwa wasichana 53, na dhumuni la mafunzo hayo ni kuwapatia maarifa ya biashara wasichana ili baada ya kuelimika waende kufundisha wasichana wenzao katika vijiji vyao kwenywe Kata wanazotoka hali itakayosaidia kubadilisha fikra na kujiendeleza kiuchumi.
“Ni Imani yetu kupitia mafunzo haya wasichana hawa wamepata elimu ya awali ya biashara itakayowasaidia kusimamia na kukuza biashara zao” alisema Shida.
Hata hivyo, Mratibu Shida aliendelea kusisitiza kwamba endapo washiriki watatumia vizuri mafunzo waliyopapewa yatasaidia takribani wasichana 795 kupata fursa mbalimbali zitakazowaingizia vipato vikubwa vyenye faida katika ujasiriamali watakaoamua kufanya kwani tumewapika kikamilifu.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzoBi. Nuru Selemani kutoka Wilaya ya Bagamoyo, kwa ujumla wamefurahi mafunzo yatasaidia kuanzisha ,kuendesha na kukuza biashara zao kwani wamefundishwa mbinu mbalimbali za kibiashara.
“wasichana wenzangu tunapopata fursa za mafunzo kama hizi msiache kushiriki kwasababu ni sehemu ya kupiga hatua”,alisema Nuru.
Nuru amedai kuwa katika siku tano za mafunzo wamejifunza mada mbalimbali kama vile kuwa wajasiriamali, namna ya kuanzisha kuendesha na kuikuza biashara, njia za kutafuta wateja na masoko. Pia wamefundishwa namna ya kupata faida katika biashara zao, faida za kilimo biashara sambamba kutambua faida na hasara za mitandao ya kijamii.
Mafunzo hayo yamehusisha wasichana mbalimbali kutoka Wilaya za kibiti, kibaha,Bagamoyo na chalinze.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.