17.08.2024.
Chuo cha Usimamizi wa Fedha IFM cha jijini Dar es Salaam kimetoa msaada wa vifaa mbalimbali kwaajili ya kusaidia waathirika waliokumbwa na mafuriko yaliyotokea kuanzia mwezi April Wilaya ya Kibiti.
Akikabidhi msaada huo Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa wa Chuo cha IFM Dkt. Eugene Mniwasa amesema misaada waliyotoa ni michango ya Wanajumuiya ya IFM, wataaluma , wafanyakazi na wasio wafanyakazi pamoja na Saccos ya IFM.
"Tukiwa sehemu ya jamii ya watanzania, Kwa uchache wetu tuliguswa,tukaona tuungane katika hili kuwashika mkono ndugu zetu, na tunaahidi kuendelea kutoa misaada ili kusaidia zaidi" Alisema Mniwasa.
Mara baada ya kukabidhiwa msaada huo Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibiti Bi. Maria Katemana aliushukuru Uongozi wa IFM kwa kuwakumbuka wakazi wa kibiti waliokumbwa na Mafuriko.
Bi. Katemana amesema amepokea penseli boksi 4, vichongeo boksi 5, kalamu boksi 9 kila Moja likiwa na kalamu 50, madaftari pisi 800, unga wa sembe kg 500, maharagwe kg 350, nguo mafurushi 17, mafurushi 3 ya viatu vya watoto, Viatu vya watu wazima pisi 228 na vifutio boksi 1.
"Tunashukuru kwa msaada huu, tutahakikisha msaada huu unawafikia walengwa wote katika vijiji vilivyoathirika kwa utaratibu utakaopangwa kupitia Uongozi wa Vijiji husika" Alisema.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Ndg. Denis Kitali amewapongeza IFM kwa kuwa na moyo wa kujitolea na kizalendo kwa ajili ya waathirika hao, kipekee akaahidi kuwa msaada huo utawafikia walengwa waliokusudiwa.
"Tunazo Kamati za maafa za Wilaya na Kamati Elekezi ambazo zitatoa maelekezo ya namna ya kugawa vifaa hivyo". Alisema Kitali.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.