Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amekabidhi gari la wagonjwa lililotolewa na Wizara ya Afya na vishkwambi 17 kwa maafisa ugani wa Idara ya Kilimo vilivyotolewa na Wizara ya kilimo.
Akikabidhi gari hilo la wagonjwa (ambulance) linalokwenda kuhudumia katika kituo cha Afya Mbwera Kanali Kolombo amesema gari hilo ni neema kwani linakwenda kuokoa maisha ya wakazi wa Mbwera na maeneo ya jirani licha ya kuwa bado kuna uhitauhitaji wa magari hayo katika vituo vya afya vilivyosalia.
"Licha ya kuwa Bado tunaupungufu wa magari hayo katika vituo vingine vitatu, kwa niaba ya wakazi wa Kibiti ninaishukuru Serikali ya Mama Samia kwa kutujali" Alisema Kanali Kolombo.
Vilevile Kanali Kolombo amekabidhi vishkwambi 17 kwa maafisa Ugani, huku akisema vinakwenda kurahisisha kazi za kitakwimu katika ngazi ya wilaya na kuanza kufanya kilimo cha ushindani katika kila kata.
"Kwa Afisa ugani ambaye kata yake itashindwa kuwa na mapato ya kutosha, nitakuwa na maswali ya kumuuliza" Alisema Kolombo.
"Kilimo ni Uti wa mgongo wa uchumi wa Kibiti, Serikali imetuwezesha vishkwambi hivi ambavyo ni kipimo tosha natarajia kuona Idara ya Kilimo inakuwa na takwimu sahihi za mazao mbalimbali wakati wote." Alisema Kanali Kolombo.
Naye Mbunge wa Jimbo la kibiti Mhe. Twaha Mpembenwe mbali na pongezi amesema ni furaha kupata gari la wagonjwa Mbwera na anakwenda kulikabidhi rasmi kwa hafla maalum. Pia Mhe. Mpembenwe amewataka maafisa ugani wote waliopokea vishkwambi, kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo.
Aidha akisoma taarifa ya mapokezi hayo Mganga Mkuu wa Wilaya Dr. Elizabeth Oming'o amemshukuru Mhe SSH na Mbunge wa Kibiti kwa kuwathamini wakazi wa Kibiti kwa kuwapatia gari hilo kwani linakwenda kurahisisha utoaji wa huduma katika Sekta ya Afya hususani maeneo ya delta na kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na watoto wachanga.
Hafla hiyo imefanyika katika viunga vya Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti na kushuhudiwa na Mhe. Mbunge wa Jimbo la Kibiti Mhe. Twaha Mpembenwe, Madiwani wa Halmshauri ya Wilaya ya Kibiti, Wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na watumishi wa Halmashauri hiyo tarehe 30.11.2023
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.