12 -13 .12. 2024.
Ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa agizo la Waziri wa nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa, Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amefanya ziara katika Kata ya Mwambao na Dimani ili kusikiliza kero za wananchi pamoja na kutembelea na kukagua miradi iliyopo.
Akizungumza na wananchi katika Kata alizotembelea, Mhe. Mkuu wa Wilaya amewaagiza wananchi katika kipindi hiki cha mvua kila kaya kulima ekari nne za chakula zitakazosaidia uwepo wa chakula ndani ya Wilaya katika kipindi chote.
Kwa upande wa mazao ya biashara amewaagiza wananchi hao kulima zaidi mazao ya ufuta na mbaazi ambayo yameonekana kushika soko lenye bei nzuri ukizingatia mazao hayo yanakubali katika Wilaya ya Kibiti bila kusahau kusafisha mashamba ya mikorosho.
Kwa upande wa Elimu amewataka wananchi hao kuhakikisha wanawaandikisha watoto wote wenye umri wa kuanza shule kuanzia miaka 4 na kuendelea kuanza darasa la Awali na Msingi bila kuwaacha nyumbani watoto wenye mahitaji maalum kwani wana haki sawa.
Kero zilizotolewa na wananchi hao ni kwa asilimia kubwa zilikuwa na mfanano ambapo walielezea uchakavu na kukosekana kwa nyumba za watumishi, upungufu wa matundu ya vyoo, ubovu wa Barabara, ukosefu wa maji ya uhakika, uvamizi wa maeneo, kero za wafugaji kulisha mashamba ya wakulima, wawekezaji kutotekeleza makubaliano ya mikataba,changamoto za umeme, uhitaji wa viongozi wa kudumu, ukosefu wa vifaa tiba, mgogoro wa mpaka kati ya TFS na Kitongoji cha Mng’aru na changamoto ya ukosefu wa shule eneo la Kikwaso.
Akijibu kero za wananchi hao Kanali Kolombo alisema kero na changamoto zao amezipokea na kuahidi kuzifanyia kazi huku akisema kwakuwa masuala mengine yanahusisha bajeti basi wasiwe na shaka kila jambo linakwenda kwa utaratibu na awamu kadri fedha zitakavyokuwa zinaingia.
Aidha Kanali Kolombo ameagiza TFS kutoa mrejesho kwenye Kamati husika katika Kitongoji cha Mnga'aru kwa ajili ya kupata majibu sahihi, akisalia Mnga'aru kuhusiana na joto ardhi ambalo huzalisha umeme ardhini ameagiza kuwepo kwa ufuatiliaji ili kupata majibu ya haraka kutokana vipimo vilivyofanywa. Pia ameiagiza Idara ya ardhi kwenda kutoa tafsiri ardhini ya kutambua mpaka wa Msindaji na Kivinja A, vilevile Idara hiyo imetakiwa kuandika barua Idara ya ardhi Rufiji kuomba kukutana kujadili mgogoro wa mpaka katika mto Ruhoi unaotenganisha Wilaya hizo.
Mbali na hayo Kanali Kolombo amemwagiza Katibu tarafa ya Kibiti, Viongozi wa Vitongoji, Mtendaji Kata ya Dimani kwa kushirikiana na Mwekezaji kufanya vikao kuzunguka shamba la uwekezaji ili kubaini wavamizi na kuwaonyesha mipaka ya mwekezaji huyo sambamba na kuwapa notisi ya siku 30 ya kuwataka kuondoka kwenye eneo hilo ambalo linamilikiwa kihalali.
Katika Kata ya Mwambao alitembelea kituo cha Afya kivinja A, shule ya Sekondari Mwambao, shule ya Msingi Mkenda na Kivija B wakati katika Kata ya Dimani ametembelea shamba la mwekezaji la uzalishaji hewa ukaa(carbon), Ujenzi wa darasa Moja la kidato cha 5 katika shule ya Sekondari Dimani, Ujenzi wa vyoo vya shule ya Msingi na Zahanati ya Mnga'aru.
Akijibu baadhi ya kero za wakazi wa Dimani, Diwani wa kata hiyo Mhe. Yusuph Mbinda amesema barabara ya Mwangia-Mnga'aru tayari imetengewa fedha kwa ajili ya matengenezo huku akisisitiza Ujenzi huo kwenda sambamba na Ujenzi wa daraja la mto Ruhoi na kudai kuwa mvutano wa msitu inaomilikiwa na TFS na wananchi tayari wameshateua Kamati na sasa wanasubiri vibali kutoka makao makuu likisimamiwa na Meneja wa TFS. Kwa upande swala la joto ardhi linalohusika na uzalishaji wa umeme ardhini wataalam walifika na kufanya vipimo bado wanasubiri utekelezaji.
Naye Diwani wa Mwambao Mh. Khatib Chaurembo alijibu baadhi za kero za wananchi wake akisema kwa upande wa maji tayari sh mil 150 zimetengwa kukarabati miundombinu ya maji na kazi imeshaanza, mil 500 zimetengwa kuhakikisha maji yanasambazwa na kuwafikia wananchi. Akisisitiza changamoto ya viongozo Mhe. Chaurembo alimuomba Mkuu wa Wilaya suala la kuwa na viongozi wanaokaimu lipatiwe ufumbuzi wa haraka kwani linachelewesha maendeleo.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.