Katika kuhakikisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 unakamilika kwa wakati, Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo akiwasilisha taarifa ya mwaka wa fedha 2023-25 kwa kipindi cha January - Juni 2023 amesema miradi yote itakuwa imekamilika ifikapo tarehe 31 mwezi disemba mwaka huu.
"Hatuna kipingamizi, fedha tumeshapokea ninaahidi miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa wilayani mpaka tarehe 31 disemba mwaka huu itakuwa imekamilika" Alisema Kanali Kolombo.
Hayo yamejiri leo Oktoba 6, 2023 katika kikao cha Halmashauri kuu ya utekelezaji wa Ilani Wilaya ya Kibiti kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
Akiwasilisha taarifa hiyo Kanali Kolombo amesema kwa kipindi cha January - Juni mwaka huu, shughuli mbalimbali zimeendelea kutekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti ilipanga kutekeleza miradi yenye thamani ya sh 8,841,173,508.00 ambapo sh 744,186,508,00 ni za mapato ya ndani na Serikali kuu.
Vilevile Kanali Kolombo amesema hadi kufikia tarehe 30 mwezi Juni mwaka huu, tayari Halmashauri imepokea kiasi cha fedha zenye jumla ya sh. 7,679, 493, 524.89 sawa na 84.50% ya fedha zilizopangwa kutekeleza miradi ya Maendeleo kutoka vyanzo vya mapato ya ndani, Serikali kuu na Wahisani.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya Kanali Kolombo amesema miradi inayoendelea kutekelezwa ni katika sekta ya Elimu, Maji, Afya, Kilimo, Ushirika, Viwanda na biashara, Mifugo, Uvuvi, Maliasili, Barabara, Nishati na Utawala bora. Pia amewashukuru Wadau wa maendeleo KOFFIH, BANK YA DUNIA, TFS, THPS NA NGO'S ambao ni sehemu ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Aidha, baada ya kupokea taarifa hiyo ya utekelezaji wa Ilani, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibiti Ndg. Juma Ndaruke amewataka watumishi wote kila mmoja kupitia Idara yake kusimamia majukumu na maelekezo kwa ufasaha kwa kufuata taratibu za kazi. Pia Ndaruke amewasisisitiza Wataalam hao kutumia vizuri fedha zinazoletwa kwa ajili ya maendeleo ili zitekeleze kwa wakati miradi iliyokusudiwa.
" Serikali imeshashatoa maagizo kuwa, hakuna fedha za nyongeza kwenye miradi, tumieni fedha hizo vizuri" Alisema Ndaruke.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri Halmashauri ya Kibiti Mhe. Ramadhan Mpendu amesema kwamba kupitia nafasi yake na Viongozi wenzake wataendelea kusimamia miradi yote kikamilifu katika Wilaya ya Kibiti kwa maendeleo ya Kibiti.
Awali kabla ya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Wilayani Kibiti, pamoja na Wakuu wa Idara na vitengo walifanya ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya Maendeleo katika Kata ya Mbuchi, Mjawa , Bungu , Kibiti Mtawanya, Mlanzi na Ruaruke ili kujionea hali halisi ya miradi na kijiridhisha kulingana na rasilimali fedha zilizopokelekwa kutekeleza miradi hiyo.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.