DED KIBITI ALONGA NA WATUMISHI IDARA YA AFYA.
ASISITIZA NIDHAMU NA UTII KUWA NGUZO YA UWAJIBIKAJI.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya kibiti Mohamed Mavura amewaagiza watumishi wa Idara ya Afya kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia taratibu na kanuni za kazi ili kuweza kuihudumia jamii inayowazunguka ipasavyo.
Amesema hayo alipokuwa katika kituo cha Afya Kibiti ikiwa ni kikao cha kawaida cha utendaji ambapo amewaonya na kuwataka watumishi kuwa na matamshi yenye lugha nzuri kwa wateja (jamii) pindi wanapowapokea na kuwahudumia huku akisisitiza madaktari na manesi (senior) wazoefu, kuwaelekeza vijana hao (Juniors) namna ya kufanya kazi na kuwasiliana na jamii wanayoihudumia.
“Kila mmoja afanye kazi kwa kufuata taratibu na kanuni kwa kuzingatia miiko ya kazi,sitaweza kuvumilia mtumishi ambaye hana nidhamu kazini” alisema Mavura.
Vilevile Mavura amewataka watumishi wote wa Idara hiyo kuheshimu Uongozi uliopo madarakani, kukubali mabadiliko yaliyopo na kuwa tayari kuendana nayo ili kuhakikisha kazi zinakwenda kama kanuni zinavyoelekeza ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa kushirikiana (team work).
“ Vunjeni makundi yanaharibu kazi ,heshimuni mamlaka iliyopo madarakani na kuitii huo ndio utumishi wa UMMA”alisema Mavura.
Hata Hivyo Mavura mbali na kumpongeza Mganga Mfawidji wa kituo hicho Dr Beatrice pia amemuagiza kuongeza kasi ya utendaji kwani kituo hicho katika ngazi ya Wilaya kinategemewa na wateja wengi kwa ajili ya huduma za kitabibu hivyo anahitaji maboresho yenye kuleta mtazamo chanya kiutendaji.Pia Mkurugenzi Mavura amemuagiza Daktari huyo kuhakikisha anasimamia ukusanyaji mapato katika Idara hiyo na Kupeleka bank Kwa usalama zaidi fedha zilizopatikana Ili baadae ziweze kuisaidia kukamilisha miradi maendeleo inayoendelea.
Daktari Beatrice Malekela anachukua nafasi ya Daktari Sospeter Eunda ambaye kwa sasa ni Daktari wa kawaida katika kituo hicho, ameachia nafasi hiyo baada ya kuomba kupumzika kutokana na changamoto za kiafya zinazomkabili
Daktari Sospeter ambaye kabla ya kuwa Mganga Mfawidhi alikuwa Daktari wa kawaida kituoni hapo, mbele ya watumishi wa Idara ya afya, Mkurugenzi Mtendaji na Mganga Mkuu wa Wilaya, amewasihi watumishi hao kumpa ushirikiano Daktari Beatrice ambaye ni Mganga Mfawidhi rasmi kama walivyokua wakishirikiana nae kwani yeye kwa sasa atakuwa Daktari wa kawaida na kazi ziendelee.
“Kwa muda niliokuwa kiongozi ,nimefanya kazi kadri nilivyoweza na sasa nimeachia madaraka huku nikiendelea kuihudumia jamii katika taaluma yangu ya udaktari,tuko pamoja kiutendaji, naomba mumpe Dr Bearice ushirikiano ili tuweze kutimiza wajibu wa kuwatumikia wananchi” alisema Daktari Sospeter.
Awali Mganga Mkuu wa Wilaya Daktari Elizabeth Oming’o akimkaribisha Mkurugenzi kuongea na watumishi alisema Kituo cha Afya Kibiti ni Kituo muhimu Kwa kutoa huduma za Afya,yeye na timu yake wanaendelea kupambana kuhakikisha huduma zote muhimu zinapatikana ikiwa ni pamoja na kusimamia miradi kikamilifu na mpaka sasa katika kituo hicho wanajenga Jengo la upasuaji ambalo kwa sasa liko katika hatua ya jamvi lengo likiwa ni kutanua na kuboresha huduma za Afya katika kituo hicho.Mwisho amelishukuru shirika la KOFFIH International kwa namna linavyokuwa mstari wa mbele kuhakikisha kituo hicho kinaboresha huduma kwa kutoa michango mbalimbali ya maendeleo.
Aidha Mganga Mfawidhi Daktari Beatrice Malekela amesema,Kwa upande wa Mapato katika kituo hicho wanatarajia kukusanya mil 10 kwa mwezi kuanzia sasa wakati huo huo akamshukuru Mkurugenzi kwa kuwatembelea huku akisema maagizo na maelekezo ameyapokea na anakwenda kutekeleza kwa kuyafanyia kazi .
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.