Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Pwani Mwakilishi wa Wafanyakazi Tanzania Bara Mhe. Dkt. Alice Kaijage, amewasili Kibiti Leo Tarehe 11.4 .2024 na kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali pamoja na fedha taslimu kwa wahanga wa Mafuriko ya maji ya mvua kutokana na kuongezeka kwa maji katika mto Rufiji.
Vifaa vilivyotolewa ni sabuni ya unga ya kufulia kiroba 1, unga wa sembe viroba 20 vyenye ujazo wa kg 5, chumvi katoni 4, mafuta ya kupaka boksi 1, sabuni ya mche boksi 1, dawa za meno dazani 1, miswaki pisi 36, majani ya chai boksi 1 yenye ujazo wa g 50 na pesa taslimu sh. 200,000 kwa ajili ya mafuta ya boti kuweza kuwafikia wahanga visiwani (delta).
Akikabidhi vifaa hivyo Mhe. Dkt. Alice amesema tangu Mafuriko yatokee mbunge wa Jimbo la Kibiti Mhe. Twaha Mpembenwe aliacha shughuli za kibunge na kuja kuungana na wananchi wake, hivyo ameona ni wakati sahihi wa kumuunga mkono mhe. Mpembenwe kwa kuwafariji wahanga wa Mafuriko hayo kwa kidogo alichojaliwa.
"Nimekuja kumuunga mkono Mhe. Mpembenwe, Kwa kidogo nilichokileta hapa kwa hawa ndugu zangu ninaamini kitawagusa kwa namna moja au nyingine kwenye mahitaji yao katika kipindi hiki" Alisema Dkt. Alice.
Vilevile Mhe. huyo amewashukuru viongozi wa Chama Tawala (W) UWT viti maalum na Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Kamati ya mapokezi kwa kuitikia wito wa kumuunga mkono katika shughuli hiyo ya kijamii.
Akipokea vifaa hivyo Mbunge wa Jimbo la Kibiti Mhe. Twaha Mpembenwe amemshukuru Mhe. Alice kwa kuonyesha moyo wa upendo, kujitoa kuwagusa wakazi wa Kibiti waliopatwa na Mafuriko, huku akiahidi kuwa msaada uliotolewa utawafikia wahanga kama ulivyokabidhiwa.
"Tunakushukuru sana Dkt Alice, umegusa maisha ya wanakibiti hasa katika kipindi hiki muhimu cha maafa ya Mafuriko" Alisema Mpembenwe.
Mara baada ya kupokea msaada huo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Ndg. Hemed Magaro kwa niaba ya watumishi wote amemshukuru Mbunge huyo kwa kujali na kuwathamini wanakibiti katika wakati huu wanaopitia kwani msaada alioutoa ni sehemu ya uhitaji wa mahitaji muhimu kwa wahanga hao.
"Msaada huu unakwenda kunusuru maisha ya wahanga katika Kata zilizokubwa na Mafuriko, hivyo niwasihi tu kwa wengine mtakaoguswa karibuni kutuunga mkono katika kipindi hiki" Alisema Magaro.
Aidha Mwenyekiti wa UWT Wilaya Mhe. Tatu Mkumba mbali na pongezi ametoa wito kwa jamii kuendelea kujitoa kuwasaidia ndugu zetu kupitia misaada mbalimbali kwani Bado kuna uhitaji mkubwa.
"Tunashukuru kwa jitihada zako kuhakikisha unatufikia kutushika mkono, ahsante sana". Alisema Mkumba.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.