Taasisi ya Pakaya inayojihusisha na mradi shirikishi wa Uhifadhi wa Misitu ya Mikoko na bayonuai nyinginezo ya Wilaya ya Kibiti, imeanza utekelezaji wa uanzishwaji wa ujenzi wa Kituo cha Utalii Ikolojia katika fukwe ya Kijiji cha Jaja kilichopo kata ya Kiongoroni Tarafa ya Mbwera.
Akizungumza na Wataalamu wa Wilaya ya Kibiti Mkurugenzi Mtendaji na Meneja mradi huo ndg. Bakari Kisoma amesema Pakaya imelenga kuendeleza wanajamii wa vizazi vya sasa na vijavyo sambamba na uhifadhi wa mazingira katika Delta hiyo ya Rufiji.
Mara baada ya kukagua eneo Hilo, Afisa Tarafa ya Mbwera Ndg. Lucas Magai amesema mradi huo utaweza kuinua vipato vya wananchi kwa ujumla, hivyo kwa manufaa hayo ngazi ya wilaya watatoa ushirikiano kuhakikisha jitihada za PAKAYA zinatekelezwa katika Tarafa hiyo.
Katika kutekeleza mradi huo Afisa Maliasili na Utalii Ndg. Dotto Mandago ameiagiza Taasisi hiyo kushirikiana kwa ukaribu na Halmashauri kwa kufuata Sheria na kuzingatia tamaduni za jamii husika.
Ili kuenzi tamaduni za Pwani Kaimu Afisa Utamaduni Ndg.Francis Kimario amesisitiza kuwa miundombinu inayojengwa, huduma na burudani zitakazotolewa ziendane na utamaduni wa eneo la Jaja.
Licha ya kupongeza shirika hilo kwa kuiona Jaja kupitia fukwe nzuri iliyopo Mwenyekiti wa Kijiji cha Jaja amesisitiza kuwepo kwa mkataba utakaoonesha namna wanakijiji hicho watavyonufaika kupitia uwekezaji huo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Meneja wa TFS Ndg, Rasuli Msuya amesema kupitia jukumu lao la ulinzi wa misitu watakakikisha urejeshwaji wa uoto wa asili unarejea hususani mbwera magharibi ambapo utekelezaji unaendelea chini ya PAKAYA
Aidha shughuli nyingine zinazoendelea kutekelewa katika mradi huo ni uanzishwaji wa ufugaji nyuki na tayari wamekwisha gawa mizinga na vifaa vya kukamulia asali katika Kijiji cha Kiongoroni na Msala.
Pia kutakuwa na vituo vya biashara ya mazao ya Pwani na bahari.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.