Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji (R) Jacobs C. Mwambegele leo tarehe 12 julai, 2023 ametembelea ofisi za Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Kibiti Bw. Hemed S. Magaro ili kukagua na kujiridhisha na maandalizi ya Uchaguzi Mdogo wa Udiwani Kata ya Mahege, Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti.
Akisoma taarifa ya maandalizi ya Uchaguzi huo, Msimamizi wa uchaguzi Bw. Magaro amemueleza Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwamba mpaka sasa hakuna changamoto yoyote iliyojitokeza na maandalizi yote yamekamilika na vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa 1:00 Asubuhi kama sheria inavyoelekeza.
"Mimi na timu yangu tumejipanga vizuri kuhakikisha zoezi hili linakamika kwa usalama" Alisema Magaro.
Aidha Bw. Magaro ameishukuru Tume ya uchaguzi kwa kufika kutoa na kushiriki mafunzo sambamba na utoaji wa vifaa ambavyo vimekamilika kwa asilimia miamoja.
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika tarehe 13 Julai 2023 yaani kesho, licha ya Kibiti pia utahusisha kata nyingine 12 ambazo ni Ngoywa iliyopo Halmashauri (W) Sikonge, Kalola iliyopo Halmashauri (W) Uyui, Sindeni iliyopo Halmashauri (W) Handeni, Potwe iliyopo Halmashauri (W) Muheza na Kata ya Kwamsheshi iliyopo Halmashauri (W) Korogwe. Nyingine ni Kata ya Bosha iliyopo Halmashauri (W) Mkinga, Bunamhala iliyopo Halmashauri (W) Bariadi, Kata za Njoro na Kalemawe zilizopo Halmashauri (W) Same, Kata ya Kinyika iliyopo katika Halmashauri (W) Makete, Magubike iliyopo katika Halmashauri ya (W) Kilosa, na Kata ya Mbede iliyopo katika Halmashauri (W) Mpimbwe.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.