Kamati ya Lishe Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti imefanya kikao cha tathmini ya hali ya Lishe Wilayani humo leo Juni 20, 2024 katika ukumbi wa Halmashauri hiyo ikiwa ni kikao chake cha robo ya 3 kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Kikao hicho kimejadili mambo mbalimbali ikiwemo kupokea ripoti ya lishe wilaya katika kipindi cha mwezi Januari hadi Machi 2024.
Akiwasilisha ripoti hiyo Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Bi. Roina Daza amesema hali ya lishe wilayani Kibiti imeendelea kuimarika kwani mikakati na utekelezaji wa shughuli za kamati ya lishe ndani ya Halmashauri imesaidia kupunguza hali ya udumavu na utapilamlo kwa wanafunzi shuleni, watoto walioko majumbani pamoja na jamii nzima kiujumla.
“Katika kipindi cha Januari-Machi, Kitengo cha lishe kimetembelea makundi mbalimbali wakiwemo Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, Wafungwa gerezani, kaya mojamoja na wanajamii wengine kupitia vikao vya wazazi, vijiji na Kata ambapo tumetoa elimu ya lishe, matibabu ya Utapiamlo kwa familia zenye hali mbaya ya lishe na kufuatilia maendeleo ya wale ambao walipatiwa matibabu ya Utapiamlo na wote wanaendelea vizuri” Alisema Bi. Roina.
Taarifa ya hali ya lishe shuleni kuanzia shule za awali hadi sekondari pia imeonekana kuendelea vizuri kwani karibu shule zote zinasimamia upatikanaji na utoaji wa chakula chenye lishe bora kwa wanafunzi wake kwa kuanzisha klabu za lishe shuleni, kilimo cha mazao mbalimbali na kuhimiza michango ya wazazi ili wanafunzi hao waweze kula.
Aidha Mratibu wa Mpango wa kunusuru kaya masikini (TASAF) Bw. Jamal Ngwire amesema TASAF imeendelea kutumia jukwaa lao la ugawaji fedha kutoa elimu ya lishe kwa kwa kaya hizo.
“Tumewaambia wananchi katika utoaji wa chakula tusibague watu kwa jinsi na jinsia, hakuna chakula cha mwanamke na mwanaume au mtoto na mkubwa, watu wote wanatakiwa kupata chakula chenye lishe bora” Alisema Bw. Ngwire.
Akitoa mchango kwa jambo hilo, Mganga Mkuu wa Wilaya Bi. Elizabeth Oming’o amesema “Tumewaomba wenzetu wa TASAF wasichoke, waendelee kutoa Elimu kwenye vijiji vyote wanavyokwenda kwakuwa katika shughuli zao za ugawaji fedha kunakuwa na mkusanyiko mkubwa wa watu lakini pia kwenye tukio hilo wanakuwa makini sana kusikiliza, hivyo Elimu ya Lishe itawafikia kiurahisi”.
Naye Afisa maendeleo ya jamii wilaya ya Kibiti Bw. Hamis Mnubi kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji ambaye ndiye mwenyekiti wa kikao hiko amewapongeza wajumbe wote kwa mahudhurio mazuri na kuwasilisha taarifa zilizonyooka na zenye matumaini kwakuwa hali ya lishe imeendelea kuimarika kiwilaya.
Pia Bw. Mnubi amewataka watendaji kata na vijiji kusimamia upatikanaji wa lishe kwa kuwashirikisha wazazi kwa ukaribu na kuwahamasisha kushiriki vikao vya lishe, utaratibu ambao utasaidia upatikanaji wa lishe kwa uhakika kwani wao ndiyo wafanikishaji wakuu lakini ndiyo wamekuwa kikwazo na changamoto kubwa kwa kutokutoa ushirikiano katika jambo hili.
“Suala la lishe ni agenda ya kitaifa kwa sasa, kwani ni jambo linalosimamiwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwenyewe akiwa na lengo la kupunguza ama kuondoa kabisa hali ya udumavu hapa nchini, basi tukalisimamie vyema” Alisema Mnubi.
Wajumbe wa kikao hicho wote kwa pamoja wamekubaliana kutekeleza yale waliyokubaliana kwa mustakabali wa wananchi wote.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.