20.08.2024
Kamati ya ugawaji wa ardhi Wilaya ya Kibiti imefanya ziara yenye lengo la kujiridhisha juu ya ugawaji wa maeneo ya malisho kwa wafugaji kwa kufuata taratibu pamoja na kupokea kero na migogoro iliyopo katika maeneo hayo.
Katika ziara hiyo Kamati ilibaini vitalu 3 katika Kijiji cha Mtunda na kitalu 1 katika Kijiji cha Uchembe vinauhitaji wa fidia kabla ya kugawiwa kwa wafugaji. Pia Kamati hiyo ilibaini Serikali za vijiji zimeridhia mpango huo.
Vilevile Kamati imeagiza wafugaji wote wenye vitalu kushauriwa kuweka mabango makubwa yenye kutambulisha vitalu husika (Ranchi ndogo), kuhakikisha utaratibu wa kuwafidia wakulima walioendeleza maeneo yao kabla ya wafugaji kumilikishwa hususani vitalu no 76A, 61A, 104 katika Kata ya Mtunda na kitalu namba 1 katika Kijiji cha uchembe.
Maagizo mengine yaliyotolewa ni kuandaa mpango wa matumizi ya vitalu vya mashamba darasa katika kila Ranchi na pia Halmashauri kuhakikisha wafugaji wote waliopatiwa vitalu wanahamishia mifugo yao kwenye vitalu husika.
Aidha Kamati imeridhia mchakato wa ugawaji wa Ranchi kuendelea isipokuwa vitalu namba 76A, 61A na kitalu namba 1 mpaka utatuzi utakapopatikana.
Kamati hiyo iliongozwa na Mwenyekiti wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Ndg. Hemed Magaro, Afisa Ardhi Mteule Bw. Zephania Sabo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Mazingira na Ujenzi ambaye ni mjumbe wa kamati ya ugawaji wa ardhi, Mhe. Yusuph Mbinda, Mhe. Zainabu Chitanda Diwani Viti Maalum, wakiwa wameambatana na Wataalam pamoja na Wenyeviti na wajumbe wa Vijiji.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.