Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo akiwa ameambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama, amepaza sauti akiwasihi wadau mbalimbali kujitokeza kuwasaidia wahanga wa Mafuriko Wilayani humo ambao kwa kiasi kikubwa hawana makazi na vyakula baada ya nyumba zao kuzingirwa na Maji na mazao kusombwa kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.
"Wadau mbalimbali,Taasisi na watu binafsi popote mlipo naomba muitizame Kibiti kwa jicho la tatu, wahanga hawa wanauhitaji mkubwa, hali si shwari kwa sasa" Alisema Kolombo.
Akizungumza kwa msisitizo Kanali ameeleza kuwa ndani ya Wilaya ya Kibiti vijiji 19 vinapatikana katika delta ya Rufiji, ambapo tayari maji ya Mafuriko hayo yamefika katika vijiji hivyo.
"Mpaka sasa tuna jumla ya wahanga 36,900 ambapo mbali na nyumba zao kufikiwa na maji wapo pia wahanga ambao mashamba yao yameharibiwa kabisa na maji tumeorodhesha wote" Alisema.
Kanali Kolombo amebainisha hayo Jana alipokuwa katika ziara muhimu yenye lengo Kuangalia Usalama wa kambi na afya za binadamu, Kukabidhi misaada iliyotolewa kwa wahanga, Kukagua njia zinazotumika kufikisha misaada, Kuangalia ukubwa wa janga na kukagua namna kambi zinavyopokea wahanga hao.
Mara baada ya kujiridhisha Mkuu huyo wa Wilaya ameifunga kambi ya shimo la Hela rasmi kwa sababu tayari imekwishazingukwa na maji na kuamuru wakazi wote kuhamia kambi ya Kitumbini ambapo ni salama zaidi na misaada itatolewa huko.
"Kuanzia sasa kambi hii naivunja hameni, kambi itakayotumika ni ya Kitumbini na misaada yote itatolewa huko na si kwingineko" Alisema.
Kanali Kolombo amewasihi wananchi kuishi kwa utulivu na kufuata maelekezo huku akiagiza Kuimarishwa kwa ulinzi na kufunguliwa kwa zahanati Kambini hapo kwa ajili ya huduma za kiafya n.k. Pia ameiagiza TARURA kuhakikisha kwa namna yeyote wanafungua Barabara ya kikale mpaka Mtunda ili iweze kurahisisha usafirishaji wa misaada sambamba kuhakikisha chakula kinagawiwa kwa walengwa na si vinginevyo pamoja na misaada mingine.
Licha ya maagizo hayo Kanali Kolombo amewataka wakazi wote wanaoishi maeneo ya delta na mabondeni kuendelea kuhama kwa haraka kuelekea maeneo yaliyoinuka na kwenye makambi kwani mvua bado zinatarajiwa kuendelea kunyesha kwa wingi.
"Kwa mujibu wa Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania, mvua zitaendelea kunyesha hadi mwezi mei endeleeni kuhama kuelekea kwenye kambi zilizotengwa hususani maeneo ya miinuko" Alisema Kanali Kolombo.
"Misaada yote itatolewa kwenye makambi niwasihi tu elekeeni kwenye kambi muweze kupata huduma, hususani kambi zilizotengwa za kitumbini, kikwajuni, mtomboli na Mkwinda" Alisema.
Akigawa misaada hiyo Kanali Kolombo ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Menejimenti ya Kitengo cha Maafa, na Mdau mmoja Dr. Alice Kaijage kwa kuwajali wananchi na kuwaletea misaada mbalimbali ambayo tayari imeshaanza kusambazwa na mingine inaendelea kusambazwa kwa wahanga.
Aidha Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kibiti SSP John Mwakalukwa akitoa Salam za pole amewataka wote wenye vitendo viovu Kambini hapo kuacha mara moja kwani jeshi la Polisi limejipanga vizuri kukabiliana na wote wenye nia ovu Kambini hapo.
Naye Inspekta Fransisco Chunji akimwakilisha kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani kutoka kikosi cha uokoaji katika Salam zake za pole amewasihi wananchi hao kuthamini maisha yao kwa kuishi kwa tahadhali kubwa na kufuata maelekezo watakayopewa na viongozi pamoja na wataalam ili kuweza kujinusuru pamoja na watoto.
Nao baadhi ya wazee wananchi wameishukuru Serikali na Mdau kwa kuwajali katika kipindi hiki, wameishukuru Kamati ya Ulinzi na Usalama kwa kuwasimamia vema na kuwafikia makabini, huku wakikiri kuwa tayari kutoka katika maeneo hayo endapo wakipewa makazi ya kudumu. Mbali na hayo wameomba kupatiwa huduma za kiafya, usafiri, maji safi na salama, vyakula, malazi na mbegu za muda mfupi ili waweze kuanza kulima upya.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.