12.12.2023
Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amefungua mafunzo ya siku tatu ( 12-14 Disemba,) ya Uongozi, usimamizi pamoja na uanzishwaji wa jumuiya za kujifunza mashuleni (JzK) yakiendeshwa na wakufunzi /wawezeshaji watatu kutoka chuo cha Uongozi ADEM Bagamoyo na Mwanza, Mratibu wa shule Bora wa Mkoa wa Pwani Bi. Oliver kapaya, mwakilishi kutoka Ofisi ya uthibiti ubora wa shule na Afisa Taaluma msaidizi Idara ya Elimu Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Mwl. Violeth Mahimbo.
Washiriki mafunzo hayo ni Maafisa Elimu Kata, Walimu Wakuu wote wa shule za msingi na Viongozi wa ngazi ya Halmashauri ambao walitangulia kushiriki mafunzo tarehe 11/12/2023.
Mafunzo hayo ni mpango mkakati wenye lengo kuwajengea uwezo Viongozi kwenye masuala ya Uongozi na usimamizi Bora uliokusudiwa kuimarisha ufundishaji na Ujifunzaji.
Akimkaribisha Mkuu wa Wilaya, Katibu Tawala wa Wilaya Bi. Maria Katemana amesema anaamini baada ya mafunzo haya, washiriki wote watakwenda kupanga na kusimamia wenzao kujitathmini ili waweze kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Aidha akifungua mafunzo hayo katika ukumbi wa shule ya wavulana Kibiti Kanali Kolombo amesema kuwa, Mtaala wa Elimu ya Msingi uliowekwa na dira ya Serikali umelenga kumuandaa Mtanzania kuwa na mtazamo chanya unaothamini usawa na elimu bila ukomo.
"Ninawashukuru walimu kwa kuitikia wito wa kushiriki na kupokea mafunzo haya hongereni sana huu ni mpango wa Mhe. Rais tunamshukuru sana".
Hata hivyo, Kanali Kolombo aliendelea kusema kuwa, licha ya matokeo ya Kibiti kutoridhisha ni wakati sahihi sasa kupitia mafunzo hayo ya uongozi kutafuta mbinu mbadala na kuongeza jitihada ili kuweza kupiga hatua zaidi.
Naye Mwl Iddi Ally, Afisa Elimu Kata wa Kata ya Mlanzi ambaye ni mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo amesema, mafunzo waliyopitishwa yamejikita zaidi kwenye kuongeza maarifa na mbinu za usimamizi wa jumuiya za kujifunza ( JzK) .
Vilevile Mwl. Iddi Ally amesema kupitia mafunzo hayo wamewezeshwa kujua umuhimu wa kujifunza, na ya kuunda muundo wa jumuiya hizo kwa ngazi za shule .
Halikadhalika amesema, kuwezeshwa kujua manufaa ya JzK katika kutatatua changamoto zinazokwamisha ujifunzaji na ufundishaji ni jambo ambalo liko ndani ya uwezo wa shule na Kata kwa ujumla.
Akifafanua kuhusu shule Bora Mratibu wa shule Bora Bi. Oliver Kapaya alisema shule Bora ni mpango na mradi wa Serikali unaofadhiliwa na Serikali ya Uingereza kupitia mfuko wa UKAID unao lenga kuinua kiwango cha elimu ya Awali na Msingi nchini. Program ya Shule Bora inatekelezwa katika Mikoa Tisa Tanzania Bara.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.