Mnada wa kwanza wa korosho msimu wa 2023 Mkoa wa Pwani umefunguliwa rasmi wilayani Kibiti Leo novemba mosi ukiwa na wazabuni 27 ambapo korosho zimeuzwa Kwa bei ya wastani ya sh. 2094.46 kwa daraja la kwanza na sh 1600 kwa daraja la pili baada ya wakulima wote kukubaliana kuuza kwa bei hiyo.
Katika mnada huo jumla kilogram 3,711,235 za korosho zilizouzwa ni za daraja la kwanza na kilogram 146,372 ni za daraja la pili.
Akizungumzia tozo zinazowahusu wakulima katika ngazi ya kimkoa na kitaifa Meneja wa COREKU Mkoa wa Pwani Hamis Mantawela amefafanua kuwa, jumla ya makato ya tozo ni 208.94 ambapo tozo ya uendeshaaji wa vyama vya ushirika ni sh. 100, tozo ya Halmshauri ni sh. 56.94, tozo ya Bodi ya korosho ni sh 25, tozo ya Tali Naliendele ni sh 25, tozo ya wadau ni sh 2 wakati tozo ya usafiri hutegemea na umbali wa Amcos.
Akifungua mnada huo Mkuu wa Wilaya ya Kibiti na Mgeni rasmi Kanali Joseph Kolombo amewaagiza wakulima vyama vya ushirika kuhakikisha wanazuia utoroshaji wa korosho ndani ya Wilaya husika, vyama vya Msingi kutoa elimu kwa wakulima na kuhakikisha havipokei korosho mbichi.
"Kwa yeyote atakaekamatwa akitorosha korosho, chombo chake Cha usafiri na mzigo wake vitataifishwa" Alisema Kanali Kolombo.
Hata hivyo amewataka wanunuzi na Taasisi za fedha kuwalipa haraka na kwa wakati wakulima ili waweze kufanya mambo yao ya maendeleo huku akisisitiza wakulima hao kuhakikisha Katika msimu huu wa mvua wanalima mazao ya chakula pia.
"Nataka katika msimu huu kila kaya kuwa na hekari nne za mazao ya chakula Wilaya ya kibiti sambamba na mazao mengine ya biashara kama vile mbaazi na nitakagua. "Alisema Kolombo.
Vilevile Meneja wa Tawi la Dar es Salam Bodi ya korosho Bi. Domina Mkangara, ametoa Rai kwa wakulima wote kuhakikisha wanaokota korosho kila siku mashambani ili kuhakikisha zinakauka vizuri na kuwa katika ubora unaotakiwa katika kipindi hiki ambacho mvua zimeanza kunyesha.
Aidha kwa niaba ya Msajili wa Vyama vya ushirika Bw. Hamas Chacha amesema, Msajili ameagiza wakulima wote kupeleka kwa wakati korosho kwenye maghala yaliyoainishwa, pia amewaelekeza viongozi wa vyama vya Msingi kushughulikia masuala ya minada mapema huku akikitaka Chama Kikuu kuhakikisha kinasimamia malipo ya wakulima ndani ya siku Saba.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.