Mkuu wa wilaya ya Kibiti kanali Joseph Kolombo ameishukuru Serikali chini ya Taasisi ya Marine Parks and Reserves Unit (MPRU) kwa kuanzisha chombo maalum cha kulinda na kusimamia matumbawe nchini Tanzania. Matumbawe yakilindwa yataongeza tija kwenye uzalishaji wa mazao ya bahari na kuimarisha ulinzi wa fukwe na rasilimali nyingine mfano mikoko, nyasibahari nk.
"Kupitia chombo hiki ninaamini ulinzi wa bahari utaimarika na mazao yataongezeka" Alisema.
"BMU ninyi ndiyo walinzi wakuu wa mazao ya bahari, tambueni Halmashauri tunawategemea ninyi katika kuingiza mapato" Alisema.
Kanali Kolombo amebainisha jambo hilo alipokuwa akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo na uelewa wanajamii takribani 73 juu ya faida za uhifadhi wa matumbawe na mazingira ya bahari na Pwani kwa ujumla.
Hata hivyo Mhifadhi Mkuu wa Bahari-Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu Ndg Godfrey Ngupula amesema kipekee ni faraja kwa Marine Park kupata miundombinu hiyo muhimu ambayo imeundwa maalumu kushughulikia na kuhakikisha ulinzi wa matumbawe baharini wakati wote.
" Katunzeni matumbawe yatutunze, awali hatukuwa na chombo hiki nchini, Marine Park tumethubutu, tunakwenda kukizindua wakati wowote kuanzia sasa kwani tuko katika hatua za mwisho za ukamilishaji" Alisema Ngupula.
Kwa upande wake Afisa Uvuvi wa Halmashauri ya Kibiti Ndg. Furaha Nyamombo yeye aliwaelimisha wanajamii namna bora za uvuvi kwa kutumia zana rafiki huku akiwaonya juu ya matumizi ya mitego isiyo salama na sambamba na faida zitokanazo na Uchumi wa Buluu kutokana na mazao ya bahari.
Aidha kwa niaba ya washiriki Bakari Chombongetwa, Fatuma Seif, Tamima Shabani, walishukuru Taasisi hiyo kwa kushirikiana na Halmashauri kwa kuwaelimisha na kuwajengea uwezo hivyo, wanakwenda kuwa mabalozi kwa jamii zao lengo kubwa likiwa ni kudumisha ulinzi na uhifadhi wa matumbawe katika maeneo yao.
Mafunzo hayo yamehusisha vikundi vinavyolinda na kusimamia rasilimali za mazao ya bahari na Pwani (BMU) Wemnyeviti wa Vijiji kutoka kata husika pamoja na Wataalam wa Halmashauri.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.