Katika kuhakikisha Miradi miradi inajengwa kwa viwango, na inakamilika kwa wakati , Kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Kibiti ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya Kanali Joseph Kolombo imetembelea na kukagua miradi 5 ya maji inayotekelezwa ndani ya Wilaya kupitia wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini RUWASA yenye dhamira ya kupunguza tatizo la uhaba wa maji kwa kiasi kikubwa mara tu itakapokamilika.
Katika ziara hiyo kamati iliwasili Kijiji cha Mjawa, ambapo walikagua mradi wa maji ya bomba wenye thamani ya sh 503,600,761.96 unaotekelezwa kwa fedha za mfuko wa maji wa Taifa (NWF) chini ya Mkandarasi M/s Trinity manufacturing services Ltd, na ujenzi umekamilika kwa 80%. Katika mradi huu kunajengwa mnara wa mita 12 utakaobeba tanki la maji lenye ujazo wa Lita 150,000 (150M3) na kazi inaendelea.
Mradi wa maji Mjawa
Vilevile walikagua mradi wa maji ya bomba wa Mahege wenye thamani ya sh 383,290,130,80 unaotekelezwa kwa fedha za Uviko 19 kwa usimamizi wa Mkandarasi FEDERICK CONSTRUCTION COMPONY LTD na mpaka sasa umekamilika kwa 90% na kazi zinaendelea. Katika mradi huu pamejengwa mnara wa mita 9 wa tanki la maji lenye ujazo wa Lita 50,000 huku ukitarajiwa kuwafikia wakazi wapatao 2731 .
Mradi wa maji Mahege
Wakiwa katika Kijiji cha mchungu ambapo pia walikagua mradi wa maji ya bomba wenye thamani ya sh 452,660,782.35 kwa fedha za mfuko wa maji wa Taifa (NWF) na kusimamia na Mkandarasi wa M/S FEDERICK CONSTRUCTION COMPANY Ltd, ambao ukikamilika utasaidia kunufaisha wananchi wapatao 1220. Katika mradi huu kunajengwa mnara wa mita 12 na tanki la maji lenye ujazo wa Lita 50,000 ujenzi upo hatua ya umaliziaji.
Pia walitembelea mradi wa maji wa Kilulatambwe wenye thamani ya sh 790,116,495,00 chini ya Mkandarasi M/S Ecia kwa fedha za mfuko wa maji wa Taifa (NWF) na kukamilika kwa ujenzi huu kutanufaisha wananchi wapatao 1033. Katika Mradi huu kunajengwa mnara wa mita 6 na tanki lenye ujazo wa Lita 50,000.
Mradi wa maji Kilulatambwe
Mwisho ziara ikahitimishwa katika Kijiji cha Mtunda penye mradi mkubwa kupita yote ambapo hujengwa tanki la maji lenye ujazo wa lita 200,000 juu ya mnara wa mita 12, wenye thamani ya sh 790,116,495.00 chini ya Mkandarasi M/S Ungando & General supplies Ltd ukitarajiwa kunufaisha wakazi wapatao 7476 katika Kijiji cha Mtunda A na B .
Mradi wa maji Mtunda
Katika miradi hiyo licha ya kujenga minara na matanki ya maji pia kunajengwa ofisi, nyumba za watumishi, vituo vya kuchotea maji, ujenzi wa nyumba za mitambo, uchimbaji wa mitaro, ulazaji na ufunikaji wa mabomba pamoja na ufungaji wa pampu za kusukumia maji.
Aidha, Mkuu wa Wilaya Kanali Joseph Kolombo, amepongeza jitihada zinazoendelea katika miradi hiyo na kuiagiza taasisi ya TANESCO kuhakikisha nishati ya umeme inafika kwa wakati kwenye miradi na kwa upande wa TARURA kuimarisha miundombinu ya barabara ambayo haiko vizuri ili paweze kupitika na kufikika kwa urahisi. Pia ameagiza kukamilisha hatua zote za umaliziaji wa Miradi zilizobakia kwa wakati huku akiahidi kufuatilia kwa karibu changamoto ya fedha za malipo ya wakandarasi hao.
Naye Meneja wa RUWASA Wilaya ya kibiti Mhandisi Pascal Kibang'ule amesema ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Kibiti na Kamati ya Ulinzi na usalama kwa ujumla katika Miradi ya Maji, imekuwa chachu ya kuamsha kasi ya utekelezaji wa Miradi ya Maji, hasa kwa jinsi alivyoonyesha ushirikiano wa kufuatilia madai ya wakandarasi yalipwe kwa wakati, na kuhamasisha utekelezaji wenye viwango. Vilevile Mhandisi Kibang’ule amesema wana Kibiti watarajie utekelezaji wa Miradi ya Maji yenye viwango, ikiendana na sera ya kumtua mama ndoo kichwani kwa kufikisha asilimia 85 ya upatikanaji wa huduma ya Maji vijijini ifikapo 2025.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.