Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amekemea tabia ya wananchi kuchoma moto mashamba yao kiholela kwani ni hatari na yanaweza kuleta madhara makubwa.
"Sipendi kabisa tabia ya kuchoma moto hovyohovyo na ninalaani kitendo hiki" Alisema Kolombo.
Kanali Kolombo amesema hayo Jumanne ya tarehe 23.07.2023 baada ya moto mkubwa kuzuka katika maeneo ya jirani na jengo la Halmashauri ya Wilaya hiyo na kuleta taharuki kulingana na miundombinu iliyokuwepo karibu na moto huo.
Hata hivyo Kanali Kolombo ameagiza kusakwa kwa mhusika aliyewasha moto huo na kufikishwa mbele ya vyombo vya Sheria.
Akishuhudia tukio hilo Mtaalam na Mshauri wa masuala ya dharura na maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Dkt. Christopher Mzava amesisitiza kuacha tabia ya kudharau moto akisema ni muhimu kuchukua hatua haraka kabla moto haujawa mkubwa.
"Moto usidharauliwe hata kidogo, hatua za awali zichukuliwe mapema kukabiliana nao lakini kuchelewa na kupuuzia kunaweza kuleta madhara makubwa zaidi" Alisema Dkt. Mzava.
Dkt. Mzava na timu yake kutoka Kitengo cha maafa Ofisi ya Waziri Mkuu wamekuwa Wilayani Kibiti kwa takribani mwezi sasa wakitoa mafunzo huhusu kujiandaa, kuzuia, kukabiliana na kurudisha hali pindi maafa yanapotokea na ghafla dharura ya moto ikajitokeza.
Kwa habari picha ni watumishi na wananchi waliofika kuhudumiwa Wilayani hapo wakisaidiana kuzima moto huo.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.