Asisitiza wajasiriamali kuchangamkia fursa ya mikopo ya 10%
06.08.2024.
Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amewashukuru wajasiriamali wa Kibiti kwa kushiriki Maonesho ya nanenane pamoja na kuonesha bidhaa zenye uhalisia zinazozalishwa ndani ya Wilaya ya Kibiti.
"Lengo la nanenane ni kuangalia je tunalima? Je tunazalisha kiasi gani cha mazao, niwaombe tu muendelee kujipanga vizuri na kuchangamkia fursa ya mikopo ya 10% inayotolewa na Halmashauri" Alisema Kolombo.
Kanali Kolombo amesema hayo kwenye Maonesho ya , nanenane Kanda ya Mashariki katika Viwanja wa Mwl. Julius Nyerere Morogoro alipotembelea na kukagua bidhaa mbalimbali katika banda la Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti.
Vilevile Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wawekezaji kujitokeza kuwekeza Kibiti kwani ni sehemu nzuri ya kuwekeza kutokana na uwepo maeneo mazuri ya uwekezaji yenye udongo wenye rutuba.
"Kibiti tuna maeneo mazuri ya uwekezaji wa kilimo, na habari njema ni kwamba tumepata mwekezaji wa kilimo Cha Alizeti ambaye tumempa Hekari 15,000.
Katika kuhakikisha mkulima huyo analima kilimo chenye tija kupitia maafisa ugani wamepima Afya ya udongo na kumshauri aina ya mbegu gwala 4 na high sun 33 zinazozaa alizeti yenye mafuta mengi, bado tunahitaji wawekezaji wengine wengi zaidi mkaribie Kibiti kwani maeneo ya uwekezaji bado yapo" Alisema.
Mbali na hayo pia Kanali Kolombo amesisitiza kilimo kuendana na utunzaji wa mazingira ambapo ameagiza viongozi kuhakikisha 50% ya miti inayopandwa iwe ya miti ya mikorosho na matunda, jambo litakalosaidia kutunza Mazingira kwa muda mrefu na kukuza uchumi kwa ujumla.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.