14.3 2024.
Wananchi wa Kata ya Mjawa na Vitongoji vyake wamejitokeza kwa wingi kuwasilisha kero mbalimbali zinazowakabili katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Mkuu wa Wilaya ya Kibiti.
Katika mkutano huo kero na changamoto zilizotolewa na wananchi hao ni ubovu wa Barabara, ukosefu wa Maji safi na salama, uchakavu na ukosefu shule, zahanati, vituo vya afya, upungufu wa rasilimali watu katika baadhi ya maeneo na utoro mashuleni.
Wakazi hao pia wamelalamika suala la wafugaji kulisha katika mashamba yao, kukaimishwa kwa viongozi wa vijiji, uwepo wa michezo ya mabonanza mitaani , kukosekana kwa kituo cha Polisi, kutaka kubadilisha mwekezaji wa bonde la kuchimba udongo uchembe n.k
Akijibu kuhusu la kituo cha Polisi, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kibiti SSP John Mwakalukwa amewapongeza wakazi wa Mjawa na wahisani kwa kujenga kituo cha Polisi ambacho mpaka sasa kimekamilika kwa 80%. Mkuu huyo wa Polisi amesema kuwa suala la ukamilishaji wanasubiri ahadi ya fedha kutoka Makao Makuu ya Polisi ili kituo hicho kimaliziwe ndiyo kianze kutumika. Vilevile amesema katika Kata hiyo kuna Polisi Kata ambaye Ofisi yake ipo katika Ofisi ya Mtendaji wa Kata na siyo katika kituo cha Polisi, hivyo kwa mwananchi yeyote mwenye changamoto zinazohitaji Polisi wanaweza kufika katika Ofisi hiyo na kusaidiwa kwa wakati. ASP Mwakalukwa pia amesisitiza wananchi kuwa na tabia ya kutoa taarifa au viashiria vya uhalifu pindi wanapohisi au kujua bila kusahau utii wa sheria bila shuruti.
Kwa upande wa maji Mhandisi Juma Ndaro amesema, mradi haujakamilika kazi inaendelea, Awali walitoa maji kwa majaribio. Mhandisi Ndaro amefafanua kuwa mwezi huu mradi huo utaanza kutoa maji kwa kutumia tanki la zamani na tayari Wana DP 14 zitakazotumika kusambaza maji majumbani wakati kwa upande wa kitongoji cha mikwara tayari visima vya maji vimeshachimbwa kwa ajili ya kukabiliana na uhaba wa maji.
Vilevile Meneja wa Tanesco Mhandisi Safari Kwibondoja akijibu kero za wananchi kuhusu umeme amesema, umeme unaunganishwa kulingana na bajeti iliyopo, changamoto ni kwamba haujamfikia kila mtu. Katika Kijiji cha uchembe Kata ya Mjawa wakati wowote kuanzia sasa nyaya zitafika na zoezi la kuunganisha litaanza mara moja japo kuwa siyo wote watapata umeme na katika shule ya Sekondari Jaribu Meneja safari amesema, wanasubiri trasfoma inunuliwe ndipo waweze kuunganisha umeme.
Pia amewataka wananchi kuwa walinzi wa miundombinu ya umeme kwani kumeibuka tabia ya wizi wa trasfoma jambo linalorudisha nyuma maendeleo ya upatikanaji na usambazaji wa umeme ndani ya Wilaya.
Hata hivyo kero ya miundombinu ya Barabara haikuachwa ambapo Mhandisi Ayubu Ngereza amewataka wananchi kuendelea kuwa wa wavumilivu kwani tayari mkandarasi amekwishapatikana na wamekwishasaini mikataba. Barabara zilizowekwa kwenye mpango ni Jaribu - Motomoto, Jaribu - Kivinja B, Mjawa - Mahege, Motomoto -Uchembe na motomoto - Jaribu.
Kuhusu kero ya mpaka wa Kibiti na Mkuranga, Afisa ardhi Ndg. Denis Kitali amesema mpaka upo changamoto ni kuwa wananchi wanaendelea kukariri mipaka ya zamani na siyo mipaka ya Sasa jambo linalosababisha kuendelea kuwepo kwa sintofahamu.
Kwa upande wa changamoto ya wafugaji Afisa kilimo, Mifugo na Uvuvi Ndg. Simeon Waryuba amesema katika kurejesha mahusiano yaliyopotea baina ya wafugaji na wakulima, Serikali ilianzisha mpango wa Ranchi ndogo ili kila mfugaji afuge na kuchunga katika eneo alilopewa bila kuingia kwa mtu mwingine. Zoezi linaendelea japo lilisimama kwa muda kutokana na malalamiko yaliyopo watawachukulia hatua wafugaji wote wanaotajwa kuwa wakorofi.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Ndg, Hemed Magaro amefafannua kwamba, mikopo inayotolewa na Serikali ilisimama kutokana na watu kushindwa kurejesha, lakini sasa itaanza kutolewa tena kwa masharti nafuu, kuhusu bonde la udongo uchembe ni swala la kisheria lipo kwa mwanasheria kutazama namna ya kubadili mwekezaji kwa sababu walikwisha kuingia mkataba wa uchimbaji wa udongo.
Licha ya hayo Mkurugenzi Magaro aliendelea kufafanua kuwa kuhusiana na upungufu wa walimu tayari kuna mpango mkakati wa kuongeza walimu mashuleni na kukarabati shule zote chakavu, huku akiwasisitiza wakazi wa uchembe kutenga hekari zisizopungua 5 ili zifanyiwe upembuzi yakinifu tayari kwa kuanza michakato ya ujenzi wa zahanati lakini wananchi wajitolee pia. Akizungumzia usajili wa shule ambazo hazijasajiliwa amesema tayari wamekwisha pokea 16,000,000 za mfuko wa Jimbo na 2,000,000 za mapato ya ndani kwa ajili ya kukamilisha majengo ili shule hizo ziweze kuombewa usajili, na kuhusu mabonanza yapo kiutaratibu yamekatiwa leseni, hivyo watoto hawaruhusuwi kushiriki mchezo huo, na endapo wakiona watoto wanashiriki watoe taarifa ili Sheria zifuate mkondo wake.
Mara baada ya kero kujibiwa na Wataalam Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo ameagiza kukamata watoto wote wanaofanya biashara na watoro, wazazi wao na wafanyabiashara wanaowatuma. Amemwagiza Mkuu wa Polisi Wilaya, Afisa kilimo na Mifugo, Watendaji wa Kata na vijiji kuwakamata na kuwachukulia hatua wafugaji wakorofi ikiwa ni pamoja na kuwafukuza endapo hawatimizi masharti. Pia Kanali Kolombo amewasisitiza wananchi wanaokopeshwa na Serikali kuhakikisha wanarejesha ili na wengine waweze kupata na kujikwamua kiuchumi sambamba na kuzibeba kero ambazo hazikujibiwa kwa ajili ya utekelezaji.
Katika mkutano huo viongozi wa Chama na Serikali wanemshukuru Mkuu wa Wilaya na viongozi wote alioambatana nao kuona umuhimu wa kufika katika Kata hiyo kusikiliza changamoto za wananchi.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.