17.09.2024.
Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amewataka wananchi kujiandikisha na kuhakikisha majina yao yapo kwenye daftari la kudumu la mpiga kura ikiwa ni sehemu ya maboresho ya daftari hilo ili kuepuka usumbufu wa kushindwa kupiga kura katika siku ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu nchi nzima.
Pia Kanali Kolombo amewasisitiza Wananchi wote wenye sifa na uwezo wa kugombea, kuchukua fomu na kugombea Uongozi huo wa Serikali za mitaa ili kufanya mageuzi ya Maendeleo.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema hayo alipokuwa kwenye ziara maalum katika Kata ya Mchukwi na Dimani yenye lengo la kuwambusha na kuhamasisha wananchi kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Mbali na Uchaguzi pia Kanali Kolombo amesikiliza, kujibu na kuchukua kero za wananchi wa Kata hizo kwa nyakati tofauti huku akiahidi kumaliza migogoro iliyopo kwa kadri itakavyowezekana.
Nao Madiwani wa Kata ya Dimani na Mchukwi walimkaribisha Mkuu wa Wilaya huyo wakisema Kata zao ni salama na zipo tayari kwa uchaguzi huo, huku wakawasisitiza wananchi wao kuwa kila anayejiona ana sifa za kuchukua fomu na kugombea achukue akagombee nafasi husika.
Awali Wananchi wakazi wa Mchukwi na Dimani walisema kero zinazowasumbua zaidi ni uhitaji wa umeme, maji, Barabara, uchakavu wa majengo ya vituo vya kutolea huduma, ukosefu wa nyumba za watumishi, upungufu wa watumishi, uhitaji wa walimu wa elimu maalum pamoja kuchelewa kwa vitambulisho na namba za askari wa jeshi la akiba baada ya mafunzo.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.