NI KATIKA MAENDELEO YA UJENZI WA SHULE MPYA 2 ZA MRADI WA BOOST.
Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo, amefanya ziara ya ufuatiliaji wa maendeleo ya ujenzi wa shule mpya 2 za kisasa, unaotekelezwa na mradi wa Boost Tanzania. Boost ni mradi unaosaidia kuboresha miundombinu ya shule za msingi na awali sambamba na dhana nzima ya ufundishaji na ujifunzaji.
Akitoa majumuisho ya ziara hiyo Mkuu wa Wilaya amewaelekeza Mkurugenzi Mtendaji, Mwenyekiti wa Miradi na Wataalam aliambatana nao, kusimamia kwa weledi mradi huo na kuhakikisha unakamilika kwa viwango na ubora unaotakiwa.
Katika maelekezo hayo pia, Kanali Kolombo amewataka wasimamizi wa miradi kuhakikisha wanawasimamia kikamilifu mafundi ili kuhakikisha wanakuwepo eneo la ujenzi kila siku, Pamoja na kufanya kazi yenye ubora wa hali ya juu ili kuondoa kabisa makosa ya kiufundi, kwani ikiwa mapungufu yatajitokeza hapatakuwa na fedha za nyongeza za kufanya marekebisho.
"Miradi yote isimamiwe kikamilifu, hapatakuwa na fedha za nyongeza, hilo lieleweke hivyo, zaidi ya hapo mtafidia wenyewe".Alisema Kolombo.
Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Ndg. Hemed Magaro amesema maelekezo yote ameyapokea na kuahidi kuyafanyia kazi kwa kushirikiana na wataalamu wake.
Licha ya kutoa pongezi kwa kazi nzuri inayoendelea, Mkurugenzi Magaro ameisisitiza kamati ya ujenzi, wasimamizi na mafundi kuongeza jitihada ya ujenzi kwa kuzingatia ubora na maelekezo ya BOQ.
Vilevile Magaro kwa nyakati tofauti, amemwagiza Afisa Elimu na Mhandisi kuhakikisha katika maeneo yote ya miradi kunakuwa na kitabu cha wageni kusaini, kuwepo na utunzaji wa nyaraka au mikataba, na stoo kwa ajili ya kuhifadhia vifaa vya ujenzi wakati kazi zikiendelea.
Aidha hali ya maendeleo ya ujenzi katika miradi yote 2 iko katika hatua ya kujenga msingi, kuweka kifusi na kumwaga jamvi kwa baadhi ya majengo na kazi zinaendelea.
Katika miradi hiyo jumla ya sh 306, 900,000/= kwa kila shule zimepokelewa ambapo kila shule kutajengwa madarasa 7, matundu 10 ya vyoo, Jengo la Utawala, kichomea taka, madarasa 2 ya awali yenye matundu 6 ya vyoo pamoja na vifaa vya michezo.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.