Zoezi uchanjaji wa chanjo ya SURUA na RUBELLA nchini limezinduliwa tarehe 15/2/2024. Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti kama ilivyo kwa Halmashauri nyingine nchini wametekeleza zoezi hilo katika hospitali ya Wilaya ya Kibiti iliyopo nje kidogo ya mji katika Kata ya Mtawanya.
Mganga Mkuu wa Wilaya Daktari Elizabeth Oming'o amesema chanjo hiyo ni muhimu sana hivyo ni vema kuhakikisha hakuna mtoto atakayekosa chanjo, kwani kwa hali ya kawaida unaweza ukaona haina maana lakini ukaja kupatwa na madhara baadaye.
"Ndg. wananchi, leo tumezindua chanjo hii , zoezi hili linafanyika nchi nzima siku ya leo hivyo msipuuze. Kibiti tutatoa huduma ya chanjo katika vituo vyote vilivyopangwa kuanzia leo tarehe 15 -18, waleteni watoto wapatiwe chanjo" Alisema Dkt. Oming’o.
Mbali na kutambua umuhimu wa chanjo Mganga huyo amewasisitiza wananchi waliofika kwenye uzinduzi huo, kuwaelimisha na kuwajulisha watu ambao hawakuweza kufika wawapeleke watoto wao wakapatiwe chanjo hiyo.
Vilevile amesema timu za uchanjaji zitakuwa katika vituo vya kudumu, vituo kuhamahama na katika maeneo mbalimbali ikiwemo maeneo ya masoko, shule, nyumba za Ibada, mashambani, vituo vya mabasi, kambi za wakimbizi, kambi za wavuvi na katika maeneo ya mipakani ambapo kuna watoto (transit sites).
Akimkaribisha Mkuu wa Wilaya kuzungumza na halaiki iliyojitokeza katika uzinduzi huo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibiti Bi.Maria Katemana amewaagiza wadau wa Afya kuendelea kuwasisitiza kinamama kuwapleka watoto kupata chanjo katika vituo vilivyopangwa kwenye maeneo yao.
Katika uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Kibiti na Mgeni rasmi katika shughuli hiyo Kanali Joseph Kolombo amesema, Serikali imejiwekea mpango mzuri wa kuhakikisha wananchi wanaishi wakiwa na Afya bora ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa chanjo za kujikinga na magonjwa kama hayo.
Kanali Kolombo amesema, lengo la kuleta chanjo nchini ni kuhakikisha wanaongeza Kinga kwa walengwa kuzuia kuenea kwa magonjwa yanayozuilikia ikiwa ni pamoja na Surua na Rubella.
"Nawasihi wazazi, walezi, baba na mama pelekeni watoto wakapatiwe chanjo, hata sisi enzi zetu tulipata chanjo kama za ndui polio n.k na tuliona mafanikio yake" Alisema Kolombo.
Surua na Rubella ni magonjwa yanayosababishwa na virusi kwa njia ya hewa. Na dalili za magonjwa hayo nyingi hushabihiana, kama vile kupatwa na homa Kali, mafua, kikohozi , macho kuwa mekundu yakiambatana na kutoa majimaji, kupatwa na vipele vidogodogo ambavyo huanzia kwenye paji la uso, nyuma ya masikio, kisha kusambaa usoni na mwili mzima.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.