Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo ameagiza Wakuu wa shule kuwapa taarifa wazazi, walezi na wanafunzi waliopata mimba wakiwa shuleni kuwasili ofisini kwake mwanzoni mwa mwezi January waweze kujadili na kutafuta mwarobaini wa utoro na mimba za utotoni.
"Majina ya wanafunzi wajawazito mnayajua, waandikiwe barua wafike ofisini kwangu baada ya sikukuu, wakiwa na wazazi wao wanieleze shida ni nini" Alisema Kolombo.
Hali hiyo imedhihilishwa na takwimu za mtihani wa kidato cha pili ambayo imeonyesha idadi ya watoto waliosajiliwa kufanya mitihani ni 2813, waliofanya mtihani ni 2593 na ambao hawakufanya mitihani ni wanafunzi 220 kutokana na sababu mbalimbali.
Hayo yamejiri tarehe 21.12.2023 kwenye kikao cha tathmini ya Elimu kidato cha pili kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti baada ya kundi kubwa la wanafunzi kushindwa kufanya mitihani na wengine kufeli.
Vilevile amewaagiza walimu kuwa na ushirikiano mzuri kuanzia ngazi za chini katika muundo wa Serikali kuhusiana na utoro na utoaji taarifa kwenye Kamati ya ulinzi na Usalama kupitia Polisi kata ili kuweza kufanya ufumbuzi wa haraka kabla mambo hayajaharibika.
Awali kabla ya Mkuu wa Wilaya kutoa maagizo hayo Wakuu wa shule kutoka shule mbalimbali walitoa taarifa za mwenendo wa elimu katika shule zao ambapo walisema chanzo cha utoro mashuleni kwa kiasi kikubwa kinahujumiwa na wazazi ambao husisitiza watoto wao kutofanya vizuri wakidai hawana fedha za kuwasomesha.
Hata hivyo Walimu hao walisema vyanzo vingine vya kushindwa kufanya mitihani kwa wanafunzi hao mashuleni vinatokana na ujauzito kwa watoto wa kike, utoro, nidhamu mbaya kati ya wazazi walimu na wanafunzi, ajira za utotoni, vigodoro, uangalizi hafifu wa wazazi kwa watoto wao na matumizi ya bangi.
Wakitoa mapedekezo ya nini kifanyike maoni mengi yamekuwa na mfanano kulingana na changamoto za kimazingira kufanana ambapo wamesema kuwa kuna umuhimu wa kuunda Sheria ndogo ndogo zitakazoweza kuwabana wanafunzi na watuhumiwa, wazazi wa wanafunzi kuchukuliwa hatua Kali, kukomesha ajira kwa watoto, kuvunja vijiwe na mageto mitaani n.k.
Shule ambazo baadhi ya wanafunzi hawakufanya mitihani ni Sekondari ya Mjawa, Zimbwini, Msafiri, Dimani, Mahege, Ruaruke, Mtanga Delta, Mtawanya, Nyamisati, Kikale, Mchuckwi na Mlanzi.
Akiwakilisha Wenyeviti wa Bodi za shule , Mwenyekiti wa Bodi ya shule ya Sekondari Msafiri Bw. Lazaro Lukonge amempongeza Mkuu wa Wilaya Kanali Kolombo kwa kuona umuhimu wa kuchukua hatua ili kupunguza tatizo lililopo ndani ya Wilaya. Pia amemuomba Kanali Kolombo kuwalinda Wakuu wa shule kwani wengi wao hufanya kazi kwa hofu na kushindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo.
Kikao hicho limehusisha Kamati ya ulinzi na Usalama, Wakuu wa shule, Maafisa elimu Kata, Maafisa Elimu Sekondari (W), Wenyeviti wa Bodi za shule na Polisi kata ndani ya Wilaya.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.