22.09.2024.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Wazazi Taifa Ndg. Ally Salum Hapi (Mnec) ameendelea na ziara yake ya kikazi Mkoani Pwani ambapo jana alifanya ziara hiyo katika Wilaya ya kibiti akiwa ameambatana na wenyeji wake wa Jumuiya pamoja na Mbunge wa Jimbo la Kibiti Mhe. Twaha Mpembenwe.
Lengo kuu la ziara hiyo ni kutembelea na Kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, kuzungumza na Wanaccm pamoja na Wananchi kupitia mkutano wa hadhara Wilayani humo.
Ndg. Hapi ametembelea mradi wa majengo ya shule za sekondari mbili ambazo ni Shule ya Sekondari Mwananchi na Shule ya Sekondari Dkt. Samia Suluhu Hassan- Lumiozi. Katibu huyo amefurahishwa na miradi hiyo huku akiwataka wananchi kupeleka watoto wao kupata elimu katika shule hizo lakini pia Walimu na wanafunzi kutunza miundombinu ya shule hizo ili ziweze kusaidia vizazi vijavyo na kusisitiza watoto hususani wa kike kusoma kwa bidii.
Mbali na hayo pia Mhe. Hapi amewataka Wazazi kuwa makini na malezi ya watoto wao bila kuamini watu wengine sambamba na kuhakikisha watoto hao wanakwenda shule na wanaodokana na adui ujinga, umaskini na maradhi.
"Wazazi tuweni makini kuhusu watoto wetu na tusimuamini mtu haswa katika malezi, tupambane na Maadui watatu ambao ni ujinga, umasikini na maradhi" Alisema.
Vilevile amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kupeleka hoja zitakazosaidia kupata fedha kwa ajili ya kununulia kemikali zitakazotumika kufanyia mazoezi ya ujifunzaji kwa vitendo (Practical) kwenye Maabara zilizojengwa katika shule hizo kwa haraka.
Aidha akiwa katika shule ya Sekondari ya Mwananchi amemuagiza Mkuu wa Wilaya hiyo Kanali Joseph Kolombo kuhakikisha ndani ya wiki Moja anahakikisha RUWASA inapeleka maji shuleni hapo.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la kibiti Mhe. Twaha Mpembenwe ameelezea kwa ufasaha Utekelezaji wa Ilani huku akiweka wazi wananchi kiasi cha pesa zilizotolewa na Mhe. Rais SSH ambazo zimetekeleza na zinaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo Jimboni humo.
Mwisho Mhe. Mpembenwe baada ya kumpongeza Mhe Rais alimuomba Mgeni rasmi kwa niaba ya wakazi wa Kibiti kufikisha salamu zao za shukrani kwa Mama Samia kwa namna alivyoithamini Kibiti na kuwapatia mabilioni ya fedha na kazi zinaendelea.
"Hatuna deni na Mhe. Rais, ila sisi tunamuahidi kumlipa kura nyingi za kishindo, tunasema Mama Samia mitano tena" Alisema Mpembenwe.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.