22.2.2024
Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amefungua warsha ya Uhifadhi wa matumbawe (mazalia ya samaki) baharini katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
"Nimefurahi warsha hii kuletwa Wilaya ya Kibiti hongereni sana kwa kuibua mradi huu muhimu katika Wilaya yangu" Alisema Mhe. Kolombo.
Kanali Kolombo amesema kwa ujumla amefurahi kupokea ujio huo kutoka Marine Parks and Reserves Tanzania, kwani ni mradi sahihi kutokana na uwepo wa rasilimali za bahari katika Wilaya ya Kibiti.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema, Matumbawe, nyasi bahari na mikoko ni vitu ambavyo havitengamishwi kutokana na umuhimu wake mkubwa katika bahari kwani faida kubwa ya matumbawe ni kuwa chanzo kikuu cha makazi na mazalia ya samaki, hivyo amewataka wananchi na wavuvi kuhakikisha wanayatunza.
"Niwasihi tu baada ya warsha hii twendeni tukaimarishe Kamati za mazingira za Vijiji vyetu ili tuweze kuhifadhi matumbawe yetu. Matumbawe ni chanzo na hifadhi ya chakula na mazalia kwa samaki na hupelekea kuwa uvunaji wa samaki wengi na ambao huongezea Halmashauri mapato" Alisema Kolombo.
Aidha, amewaagiza wavuvi kujiunga katika vikundi vidogodogo katika maeneo yao ili waweze kupewa mikopo na boti za uvuvi halali na kuachana na vitendo vya uvuvi haramu unaosababisha hasara ya kupoteza rasilimali za bahari.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Kibiti ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti kupitia uongozi wake kukubali kupokea mradi huo muhimu wenye fursa za maendeleo ndani ya Wilaya huku akisisitiza wanawarsha wote kuhakikisha wanasimamia vizuri mafunzo waliyopata ili yakalete tija katika kwa familia mojamoja na Wilaya kwa ujumla.
Naye Diwani wa Kata ya salale Mhe. Abdallah Ndomondo akimwakilisha Mwenyekiti wa Halmashauri amesema, wanaimani kubwa na mradi huo kwani ni kiashiria cha kuanza na kuimarisha uhifadhi wa matumbawe Kibiti, na kupitia mradi Wananchi wa Wilaya ya Kibiti watanufaika mno, Hivyo Madiwani wameupokea vizuri na wako tayari kutoa ushirikiano.
Hata hivyo amesema, ili kuhakikisha uhifadhi huo unadumu kuna umuhimu wa kuhakikisha elimu inatolewa kwenye jamii za vijiji vya ukanda wa Pwani ili waweze kuelewa faida za uhifadhi huo.
"Elimu hii iliyotolewa leo ni muhimu sana ikitolewa kwa wananchi na viongozi wa ngazi zote hususani ukanda wa Delta ili kila mmoja awe na uelewa juu ya uhifadhi wa matumbawe.”
Pia amewasisitiza kutoa mwongozo wa uhifadhi wa Matumbawe ambao utawezesha Vijiji kutunga sharia ndogo zitakazosaidia kuibana jamii kuogopa kufanya uharibifu wa matumbawe katika maeneo yao.
Awali alipokuwa akitambulisha mradi huo, Mkurugenzi wa Marine Parks and Reserves Tanzania Bw. Godfrey Ngupula amesema kilichowavutia kufika Wilayani Kibiti na kutaka kuimarisha uhifadhi wa Matumbawe ni uwepo wa Fukwe yenye miamba muhimu inayostahimili mabadiliko ya hali ya hewa.
"Katika km 75.5 za fukwe za kibiti miongoni mwao km 33.3 ni miamba ambayo ni Matumbawe, tunahitaji sana kuhifadhi rasilimali hii muhimu kwakuwa ni adimu sana duniani" Alisema Ngupula.
Aidha, amesema lengo kubwa la kufanya warsha hiyo ni kutaka kujua changamoto zilizopo kwenye maeneo inapopatikana miamba hiyo na kuona nini kifanyike baada ya kuzungumza na wananchi.
Mbali na hayo amewataka wananchi na Wavuvi kwa ujumla kuacha tabia ya uvuvi haramu kwani uvuvi huo husababisha kuuwa samaki na mazalia yake kwa ujumla ikiwemo Matumbawe.
Akifunga warsha hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Afisa kilimo, mifugo na uvuvi Bw. Simeon Waryuba amesema, Sasa ni wakati wa Wilaya ya kupiga vita uvuvi haramu na kuimarisha uvuvi halali, pia amefurahia sana ujio wa mradi huu na anaona namna Idara anayoisimamia inavyokwenda kuongeza mapato.
"Niwapongeze washiriki wote kwa kushiriki, sambamba na waandaaji wa warsha hii, jukumu letu ni kutoa huduma tuwaahidi tu tunakwenda kusimamia mradi huu ukawe wenye kuleta tija kwa kila mmoja". Alisema Bw. Waryuba.
Mkutano huo umehusisha watu mbalimbali kama vile Kamati ya ulinzi na Usalama, Wakuu wa Idara na Vitengo, Wakuu wa Taasisi, Waheshimiwa Madiwani, Maafisa Tarafa, Viongozi wa Dini na Chama, Wavuvi, Watendaji wa Vijiji na viongozi wa BMU kutoka maeneo ya Delta Wilaya ya Kibiti.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.