25.06.2024
Wakuu za Wilaya za KIBITI na MAFIA wakiwa na Kamati za Ulinzi na Usalama kutoka pande zote wamefanya ziara ya ujirani mwema ikiwa ni pamoja na kujadili masuala ya usafirishaji katika bandari muhimu ya Nyamisati.
Mara baada ya kuwasili katika bandari hiyo Mwakilishi wa Meneja wa bandari ya Nyamisati Bw. Abubakar Rashid Bakari alielezea changamoto mbalimbali wanazokabiliwa nazo kama vile uchache wa meli kwani iliyopo haikidhi mahitaji ya wateja wao, kutokuwa na muda sahihi wa meli kufika na kuondoka, ufinyu wa eneo la abiria kusubiri usafiri, n.k
Wakiwa katika Kijiji cha Nyamisati mara baada ya kutembelea sehemu mbalimbali ndani ya bandari walisikiliza pia changamoto na kero kutoka kwa wananchi ili kuweza kutafuta mwarobaini katika bandari hiyo.
Baada ya kikao kufanyika Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amesema kwa pamoja wameazimia kuongeza na kutengeneza meli ya songosongo kwa haraka ili ianze kutumika na kupunguza adha ya msongamano wa watu bandarini, ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu yote ya bandari.
Aidha Mkuu wa Wilaya ya Mafia Bi. Aziza Mangosongo amesema lengo la ziara yao ni kujadili mustakabali wa usafiri wa abiria na mizigo kutoka Nyamisati kuelekea Mafia na hii ni baada ya kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu changamoto wanazopitia bandarini hapo.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya amebainisha kuwa baada ya majadiliano wameazimia mengi na kuafikiana kwa pamoja kutengeneza meli ya songosongo ili kuweza kupunguza msongamano wa watu na kufanya meli kuwa 2 jambo litakalorahisisha usafirishaji wa mizigo ambayo mara nyingi huchelewa kusafirishwa, kuongeza jengo la abiria kusubiri usafiri, namna nzuri ya kukata tiketi mapema, pamoja na kukumbushia utengenezaji wa Barabara kutoka Bungu hadi Nyamisati ambayo tayari iko kwenye bajeti.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.