24/4/2023.
Wakati ulimwengu ukiadhimisha siku ya chanjo, Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti imeadhimisha kiwilaya katika Kituo cha Afya Kibiti na kuendesha zoezi la utoaji chanjo ya Polio na Kifua kikuu kwa watoto wachanga wenye umri chini ya miaka 5 na chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi kwa watoto wa kike wenye umri wa kuanzia miaka 14.
Siku hii huadhimishwa kila mwaka wiki ya mwisho ya mwezi Aprili, na zoezi la utoaji wa chanjo zote linafanyika katika vituo vyote vya afya katika kila mkoa na wilaya zake.
“Wiki ya chanjo imeanza Leo April 24 na itaendelea mpaka April 30 jitokezeni kupata chanjo” alisema Frank Patrick Mratibu wa chanjo Wilaya ya Kibiti.
Vilevile Mratibu wa chanjo ndg. Frank Patrick amesema, lengo la wiki ya chanjo duniani ni kuhamasisha jamii kuhusu kutambua umuhimu wa chanjo, kwani chanjo husaidia kujikinga na magonjwa mbalimbali ya hatari. Hivyo chanjo husaidia kupunguza idadi ya vifo vinavyozuilika kwa chanjo.
Maadhimisho haya yenye kaulimbiu isemayo “Tuwafikie wote kwa chanjo”yakichagizwa na ujumbe usemao “Jamii iliyopata chanjo, jamii yenye Afya” kwa mwaka huu Kitaifa yanaadhimishwa Katika Mkoa wa Manyara.
Hata hivyo Frank amesisitiza wananchi kujitokeza kupata chanjo ya Uviko 19 awamu pili (booster dose) ili kuendelea kujiwekea ulinzi hata kama mtu alikwisha kuchanjwa awamu ya kwanza au ya pili.
Aidha Katibu Tawala wa Wilaya Milongo Sanga kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya Kanali Joseph Kolombo, amewapongeza kina mama wenye watoto wachanga na mabinti wa kuanzia miaka 14 kujitokeza kwa ajili ya kupata chanjo kwani ni sehemu ya kuimarisha afya kwa ujumla.
“jitokezeni kupata chanjo, zoezi hili ni endelevu, hakikisheni mnalinda afya zenu”.Alisema Sanga.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.