Mkoa wa Pwani umeanza uhamasishaji wa uwekezaji katika zao la muhogo ili kuwawezesha wakulima kujiongezea kipato sambamba na kuendana na soko la China ambapo Tanzania imepata fursa kuuza mihogo nchini humo.
Hali hiyo imebainika mwishoni mwa wiki wakati maofisa kutoka Wizara ya Kilimo walipotembelea mkoa huo ikiwa ni mkakati wa wizara kuhamasisha ulimaji zao la muhogo na kuangalia changamoto zake kwa lengo la kuongeza tija na uzalishaji wa zao hilo.
Akielezea harakati za wilaya ya Kibiti katika kuhamasisha zao la muhogo Afisa Kilimo wa Wilaya hiyo Bw. Bwenda Ismail Bainga alisema, uhamasishaji huo unaenda sambamba na utoaji mafunzo, utoaji mbegu bora kwa wakulima pamoja na kuhakikisha kila kaya inakuwa na hekari moja ya muhogo jambo litakaloongeza uzalishaji. Kwa mujibu wa Bainga sasa hivi zao la muhogo katika wilaya ya kibiti limekuwa la kibiashara na hali hiyo inatokana na usafirishwaji wa muhogo mbichi kwa wingi kila siku kutoka wilaya hiyo kuenda Dar es salaam.
Alisema kuwa, hatua nyingine inayofanywa na halmashauri ya wilaya ya Kibiti ni kusaidia wakulima katika uuzaji muhogo hasa baada ya kubainika wakulima katika wilaya hiyo wamekuwa wakipunjwa wakati wakuuza mihogo kwa wafanyabiashara na sasa wilaya imejenga soko la pamoja lililogharimu milioni 65 na mategemeo ya wilaya ni kuwa mihogo utauzwa kwa vipimo stahiki tofauti na sasa ambapo wakulima wanapunjwa kwa mihogo kutenganishwa ile mikubwa na midogo.
Afisa kilimo huyo wa wilaya ya Kibiti alisema, uhamasishaji umewekwa pia katika ujenzi wa viwanda lengo likiwa kuhakikisha mihogo inanunuliwa kutoka kwa wakulima unasindikwa sambambana kuhakikisha Wilaya ya Kibiti m inatenga maeneo kwa ajili ya matumizi bora ya ardhi, wawekezaji wakubwa, wakati na wadogo pamoja na maeneo kwa ajili ya vijana na msisitizo ukiwa kila Kata itenge eneo.
Kwa sasa Wilaya ya Kibiti imekamilisha sheria ndogo ambapo kila kaya itatakiwa kulima zao la muhogo jambo litakalosaidia kusukuma watu kuingia shambani ikiwemo vijana ambapo sasa watalazimika kuingia katika kilimo ili kuendana na kasi ya Tanzania ya viwanda na soko la China la muhogo kwa kuzalisha kiasi cha kutosha.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.