Idara ya Afya, Ustawi wa jamii na Lishe ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti imefanya kikao cha siku 2 ili kutathmini hali ya Utendaji kazi wa Idara hiyo kwa mwaka uliopita. Kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Halmashauri tarehe 05 na 06 Septemba, 2024.
Akitoa neno la utangulizi mbele ya mgeni rasmi wa kikao hicho, Maganga Mkuu (W) Dkt. Dismas Masulubu amesema lengo la kikao hicho ni kufanya mapitio ya takwimu mbalimbali kwa pamoja ili kujua mahali walipotoka na walipo, kubaini changamoto na kuweka mikakati.
Lakini pia alisema kikao hicho kitawawezesha wafawidhi kubadilishana Uzoefu na kuchukua hatua za kufanya maboresho katika afua ambazo kituo hakifanyi vizuri.
“Kikao kinatoa fursa kwa CHMT na Wafawidhi kuona umuhimu wa matumizi ya ukusanyaji wa takwimu kwa ubora wake, kuziingiza kwenye mifumo rasmi na kuzichakata kwaajili ya kufanya maamuzi pamoja na kutoa fursa ya kujengeana uwezo na mbinu mbalimbali katika kuboresha huduma mahala pa kazi” Alisema Dkt. Masulubu.
Baada ya kusikia Ikama ya Watumishi katika idara hiyo kama ilivyowasilishwa na Katibu wa Afya, Makamu mwenyekititi wa Baraza la Madiwani Kibiti Mh. Omary Twanga alisema:
“Nilikuwa na maneno mengi ya kuwaambia leo kutokana na malalamiko ya Wananchi lakini kwa hiki nilichosikia na kuona leo nimeishiwa maneno yote. Kwasababu kama kituo kinatakiwa kuwa na Watumishi 10 na sisi kwetu kuna 2 au 1 lazima utoaji wa huduma uwe wa kusuasua, lakini pamoja na hayo tunawaomba sana Watumishi wetu endeleeni kuchapa kazi kwa bidii, sisi madiwani tutawaelewesha Wananchi na tunaahidi ushirikiano wa kutosha kwenu”.
Kikao hicho pia kimehudhuriwa na wadau mbalimbali wa Afya kama vile ANJITA, PASADA na THPS ambao kwa pamoja walielezea majukumu yao na namna wanavyoshirikiana na Serikali na Idara ya Afya katika utoaji wa huduma kwa Wananchi.
“Tunashukuru kwa kuona umuhimu wetu hivyo kutupa nafasi kushiriki kwenye kikao hiki, kwakuwa wadau tunatoa huduma na misaada kule kwa wananchi ni wengi tunaomba Mganga Mkuu utukusanye kwa pamoja ili kuweka mikakati tusiwe tunatoa misaada inayofanana. Kama mmoja ameleta daftari basi mwingine alete nguo hapo tutakuwa tumewasaidia sana” Alisema mwakilishi wa PASADA.
Akiongea kwa niaba ya Mgeni Rasmi Afisa Tarafa wa Kibiti Bw. Salim Mzaganya amesema ni wakati sasa Watoa huduma wa Afya kuwa na mifumo rafiki ya utoaji wa huduma inayoendana na ukuaji wa teknolojia, kwani Ulimwengu umeshahama kutoka kwenye mifumo ya Analogi na sasa tupo kwenye dunia ya kidigitali.
“Idara ya Afya ni moja ya maeneo yenye malalamiko mengi kule kwa wananchi, nawaomba sana watoa huduma jitahidini kutoa huduma bora. Yale yote mnayofanya kule sirini sisi yanatufikia hadharani, kwahiyo kama ilivyo kauli mbiu ya kikao chenu huduma bora kwa wananchi wa Kibiti ndo ikawe kipaumbele chenu” Alisema Bw. Mzaganya.
Aidha Bw. Mzaganya alifunga kikao hicho kwa kuwaasa wataalam hao kwenda kutoa huduma kwa weledi wa hali ya juu, kutoa taarifa kwa wakati pale mtu anapojaribu kuwaingilia katika taaluma zao na mwisho kabisa kusimamia na kutunza vyema miradi inayokwenda kwenye vituo vyao.
Mwisho, Idara imetoa zawadi ya vyeti vya pongezi kwa vituo vyote vya kutolea huduma za Afya vilivyofanya vizuri katika nyanja mbalimbali ikiwemo kusimamia vizuri mapato ya vituo kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.