Halmashauri ya wilaya ya Kibiti chini ya Idara ya Maendeleo ya jamii na Taasisi mbalimbali za kisheria imehitimisha siku 16 za kupinga ukatili kwa wanawake na watoto ambayo ilianza Novemba 25 mpaka disemba 10 ulimwenguni ikiwa ni siku ya haki za binadamu Duniani.
Akimkaribisha Mgeni rasmi Afisa maendeleo ya jamii wa wilaya Khamisi Mnubi amewapongeza wote waliojitokeza kukamilisha siku 16 za kupinga ukatili wa kinjinsia ambapo ni kumbukizi ya mauaji ya kikatili ulimweguni kote.
Kilele cha maadhimisho hayo kimefanyika katika jengo la kupumzikia abiria katika stendi ya mabasi Wilayani humo ambapo mgeni rasmi alikuwa Diwani wa Kata ya Kibiti Mhe. Hamidu Ungando. Katika maadhimisho hayo amesema suala la ulinzi wa watoto na wanawake ni mtambuka hivyo kila mwananchi anawajibu wa kuwalinda wanawake Pamoja na Watoto. Pia amewataka wanawake na watoto wenyewe kuwa majasiri na kutoa taarifa pindi wanaposikia au kushuhudia vitendo hivyo ili taratibu za kisheria zifuatwe mara moja kwa wote wanaohusika na vitendo vya ukatili kwa makundi hayo.
Akisoma taarifa ya maadhimisho hayo, Afisa maendeleo ya jamii anayesimamia watoto na wanawake Agness Willa amesema migogoro ya ndoa ni chanzo kikubwa cha ukatili wa watoto. katika wilaya ya Kibiti 2021-2022 matukio 24 ya ubakaji yaliripotiwa, watoto 62 walitelekezwa, 27 walijeruhiwa Kwa vipigo na 84 walitambuliwa wakifanya biashara katika maeneo ya stendi huo ni ukatili pia.
Vilevile Afisa ustawi wa jamii Kata ya Kibiti Bi Hajrat Kidua ametoa rai Kwa jamii Kwa ujumla kuwajibika kupambana na masuala mazima ya ukatili wa kijinsia kwa kuendelea kutoa elimu kwenye majukwaa mbalimbali. Pia kuijengea jamii uwezo kujua mifumo ya ulinzi na utetezi wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na kujua maeneo husika ya kutoa taarifa wanapokutana na changamoto hizo.
Aidha Jovita Mlima askari polisi kutoka dawati la jinsia ,yeye amewahimiza watoto na wazazi kutoa taarifa Kwa wakati kwani bila kutoa taarifa ni vigumu kutambua ukatili unaofanyika majumbani.
Naye Mwenyekiti wa Kata ya Kibiti, ameeleza kuwa unyimwaji wa chakula ni sehemu ya ukatili pia, amewataka wazazi na jamii kwa ujumla kulima mazao ya muda mfupi na kujiandikisha kupata mbolea mapema ili waweze kulima na kupata mazao ya kutosha, jambo litakalosaidia kupunguza utumikishwaji wa watoto (vibarua).
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.