Halmashauri Wilaya ya Kibiti imeadhimisha siku ukimwi duniani Katika Kijiji cha Mbwera Mashariki kitongoji cha Kimbumburu arimaarufu dadago la dagaa na kunogeshwa na kauli mbiu isemayo KIBITI BILA UKIMWI INAWEZEKANA.
Mratibu wa kamati ya Ukimwi Wilaya ya Kibiti Rehema Miraji amesema wameamua kuadhimisha maeneo hayo yenye shughuli za uvuvi ,kwa sababu ni maeneo hatarishi ambayo ni muhimu sana kupata elimu ya ugonjwa wa ukimwi kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu.
Bakari Mgagi ni Mwenyekiti wa watu wanaoishi na VVU Wilaya ya Kibiti, katika halaiki ya maadhimisho hayo amewatia moyo wananchiwanaoishi na maambukizi ya VVU na kuwataka ambao bado hawajatambua afya zao wapime ili ikiwa watakutwa na maambukizi wasisite wachukue hatua ya kuanza dawa mara moja kwani yeye ana zaidi ya miaka 7 anaishi na VVU alipima akajitambua anatumia dawa na maisha yanaendelea kama kawaida.
” pimeni afya zenu bila uwoga kwani kuwa na VVU na ukimwi siyo mwisho wa maisha au kufa ukifuata taratibu unaishi” alisema Mgagi.
Akimkaribisha Mgeni rasmi Mwenyekiti wa kamati ya ukimwi Wilaya Omary Twanga amesema lengo la kamati ni kuhakikisha wanaifikia jamii Katika maeneo mbalimbali kutoa elimu, ushauri nasaa na kuelekeza njia sahihi ya kujiepusha na maambukizi kwa kuchukua tahadhali kwani ugonjwa huu bado upo ndiyo maana maadhimisho ya mwaka huu wamefanyia Kimbumburu.
Pia amewata wananchi kuwa tabia ya kujitokeza kupima ili wajue uhakika wa afya na kuishi kwa amani huku akisisitiza kuacha tabia ya unyanyapaa unapojua mwenzio ameathirika.
Kwa upande wa Mgeni rasmi Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Mhe .Ramadhani Mpendu Katika maadhimisho hayo amesema, mbali na takwimu kuonyesha maambukizi ya ukimwi yamepungua ukimwi upo na bado Kuna wanaopoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa takwimu, hali halisi ya kiwango cha maambukizi kimepungua kutoka asilimia 5.9 mwaka 2012 Hadi asilimia 5.5mwaka 2017 na mpaka mwaka huu 2022 .
“ukimwi bado ni janga Kila mmoja anawajibu wa kuchukua tahadhari ya kujikinga na maambukizi ya ukimwi” alisema Mhe. Mpendu.
Vile vile Mhe. Mpendu amewaagiza viongozi wa Wilaya kupitia ngazi husika kuweka mikakati na vipaumbele ili kudhibiti maambukizi mapya ya VVU na kuifanya kibiti bila ukimwi iwezekane kama kauli mbiu yetu ya mwaka huu isemavyo.
Hata hivyo Mhe. Mpendu ambaye pia ni Diwani wa kata ya Bungu amewasisitiza viongozi na wataalamu kuendelea kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi vvu/ UKIMWI bila kuchoka, ili kutengeneza mazingira ya mtu kujitambua katika jamii.
Katika hatua nyingine Mhe. Mwenyekiti ametoa rai kwa wataalam wanaojihusisha na zoezi la upimaji na kutoa elimu kuwa na lugha nzuri pindi wanapowahudumia wananchi kwa kuwatia moyo na siyo kuwakatisha tamaa.
Aidha, Mhe. Ramadhani Mpendu ameziagiza kamati za UKIMWI ngazi ya Kata, vijiji na mitaa kupunguza maambukizi ya UKIMWI ,kwa kutoa ujumbe wa tahadhali ya kujikinga na ukimwi kabla ya kuanza shughuli zao hususani katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu kama eneo la dadago la dagaa lilivyo na mwingiliano wa watu.
Mwisho Mgeni rasmi Mhe.Mpendu amewataka wakazi wa Kimbumburu kuhakikisha wanalipa Kodi na ushuru kwa maendeleo ya Wilaya ya Kibiti kutokana na shughuli wanazofanya katika eneo hilo. Pia amewasisitiza wazazi kuwaandikisha mapema watoto ili mwakani waanze shule.
Maadhimisho hayo ambayo Ki-wilaya yamefanyika katika Tarafa ya Mbwera kitongoji cha Kimbumburu yaliambatana na zoezi la kutoa elimu, kupima, kupewa kinga (kondom) tiba (kutoa dawa) ,kutoa chanjo ya polio na uviko 19 ambapo awali siku Moja kabla ya maadhimisho (30 Novemba 22) liliendeshwa zoezi la huduma za jamii vijijini kwa uratibu wa shirika la kimataifa la Korea KOFIH
Katika zoezi la upimaji Mganga Mkuu wa Wilaya Elizabeth Oming’o amefurahishwa na mwitikio mzuri kwani sasa jamii imeona na kutambua umuhimu wa kupima ambapo zaidi ya watu 500 wamejitokeza kupima .
Katika hatua nyingine shirika la THPST lilitoa elimu ya kipimo kipya cha kujipima mwenyewe mahali popote Maarufu kwa JIPIME(self test) huku wakisisitiza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha wanakua na afya Bora kwa kupima na kujitambua.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.