Siku ya upandaji miti kitaifa huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 1 Aprili, Kampeni hii ilianza mwaka 1999 ikiwa na lengo la kutoa hamasa kwa wananchi kupanda miti na kuiendeleza misitu. Maaadhimisho ya siku hii Kimkoa na Kiwilaya hutegemea na kiwango cha unyevu kilichopo katika ardhi kufuatia na mvua. Hivyo kwa Mkoa wa Pwani mwaka huu 2024 maadhimisho haya yamefanyika jana tarehe 09 Aprili 2024 kwa kupanda miti katika Shule ya msingi Kibiti iliyopo Wilayani Kibiti.
Akisoma risala kwa mgeni rasmi Afisa misitu mkoa wa Pwani Bw. Pierre Protas amesema Mkoa wa Pwani ulifanikiwa kupanda miti 8,876,640 kwa mwaka 2022/2023 na inatarajia kupanda jumla ya miche 10,436,494 kwa msimu huu wa mwaka 2023/2024 ambayo imezalishwa na inaendelea kupandwa katika maeneo mbalimbali.
Akimuwakilisha mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amesema anawashukuru sana wananchi wote wa Kibiti na Mkoa wa Pwani kwaujumla kwa kujitokeza kushiriki zoezi hili la kuupanda miti katika eneo la shule ya msingi Kibiti.
“Zoezi hili la upandaji miti mashuleni ni endelevu na linaunga mkono Kampeni ya ‘SOMA NA MTI’ iliyozinduliwa Januari, 2022 kwa lengo la kuhamasisha wanafunzi juu ya umuhimu wa kupanda miti” Alisema Kanali Kolombo.
Vilevile Kanali Kolombo alisema zoezi hili ni muhimu sana ili kupunguza kutokea kwa athari za mabadiliko ya tabia ya nchi kama vile ongezeko la joto, mvua zisizotabirika na za uhakika pamoja na vimbunga.
“Upandaji miti na utunzaji wa mazingira ni suluhu pekee yenye uhakika wa kutunusuru na majanga haya, ndiyo maana tunasisitiza upandaji miti na kauli ya mwenge wa uhuru mwaka huu 2024 inahimiza hivyo kwa kusema ‘Tunza mazingira shiriki uchaguzi wa serikali za mitaa kwa ujenzi wa taifa endelevu ‘” Alisema Kolombo.
Akihitimisha hafla hiyo kanali Kolombo amewataka Viongozi wa Wilaya, Halmashauri na TFS kuhakikisha misitu iliyohifadhiwa inatunzwa vizuri ikiwa ni pamoja na kuzuia shughuli yeyote ya kibinadamu ndani ya misitu kama vile uchomaji wa mkaa, uvamizi wa mifugo, uchimbaji wa mchanga, kokoto, kilimo na makazi kwenye misitu mambo yanayochangia uharibifu wa misitu kwa kiwango kikubwa.
Jumla ya miti 1030 (1000 ya mbao na 30 ya matunda) imepandwa jana kataika maadhimisho haya.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.