# VITENDEA KAZI KUTOKA TAMISEMI NA WIZARA YA KILIMO.
Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amekabidhi jumla ya pikipiki 20, ambapo 6 kati ya hizo zimetoka Ofisi ya Rais Tamisemi maalumu kwa ajili ya watendaji kata na 20 kutoka Wizara ya Kilimo kwa ajili ya Maafisa Ugani katika Kata mbalimbali.
Akikabidhi pikipiki hizo Kanali Kolombo amewataka Maafisa ugani na watendaji wa kata hao kutumia vizuri vitendea kazi walivyopokea kwa kuhakikisha wanawafikia walengwa (wananchi) kwa wakati na kusisitiza kwamba hatarajii kusikia malalamiko kutoka kwa wananchi kuanzia sasa.
“Hakuna kisingizio tena wala sitarajii kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi, nendeni mkafanye kazi” alisema Kolombo.
Katika makabidhiano hayo Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Ramadhan Mpendu amesema, pikipiki hizo zilizopokelewa zinakwenda kupunguza changamoto zilizokuwepo huku akiwaagiza Maafisa ugani kuzitunza vizuri na kuhakikisha wanawafikia wakulima kwa wakati.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Mohamed Mavura, alitoa ufafanuzi kwamba kati ya pikipiki 20 zilizopokelewa 14 zilizokabidhiwa kwa Maafisa ugani zinatoka wizara ya kilimo na 6 zilizokabidhiwa kwa watendaji kata zinatoka Ofisi ya Rais Tamisemi.
Vilevile Mavura amewakumbusha wataalamu hao kuhakikisha pikipiki hizo zinatumika kwa kazi zilizokusudiwa ikiwa ni pamoja na kuzitunza vizuri . Pia Mavura amesema kupitia pikipiki hizo ni matarajio yake zinakwenda kupunguza uhitaji uliokuwepo awali Pamoja na wananchi kupata huduma zinazo stahili.
“ mzitunze na kuwahudumia wananchi, msitumie kwa matumizi yenu binafsi wala kuzigeuza bodaboda za biashara. Alisema Mavura.
Aidha Farida Lawrence na Mpore Chuma kwa niaba ya maafisa wengine wamemshukuru Rais Mama Samia suluhu Hassan na Wizara ya kilimo kwa kuwaletea vitendea kazi hivyo, kwani vitasaidia kuwafikia wakulima mashambani kulingana na jiografia ya maeneo wanayoishi na wanategemea uzalishaji wa ufuta, korosho na mazao ya chakula utaongezeka zaidi kwani wamejipanga kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi Ili waweze kuzalisha mazao kwa wingi.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.