Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuboresha Sekta ya Kilimo na kuhama kutoka kwenye kilimo siasa (political Agriculture) na kuelekea kilimo cha kiuchumi (Economic Agriculture) lengo likiwa ni kumsaidia mkulima kuzalisha mazao yenye tija ili kuweza kumudu soko la kimataifa na kuboresha maisha binafsi.
Chalamila amesema hayo Julai 19, 2024 alipokuwa akiendesha kikao cha maandalizi ya sherehe za nanenane 2024 Kanda ya Mashariki kilichofanyika katika viwanja vya Julius Nyerere vilivyopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ambapo maadhimisho hayo yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Agosti Mosi hadi Agosti 8 mwaka huu.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema lengo la maonyesho hayo sio tu kuwaonensha Wananchi bidhaa, vipando vya mazao mbalimbali, mifugo, uvuvi na teknolojia za kisasa lakini pia Wananchi watapata fursa ya kuuza bidhaa zao na ameitaka kamati ya maandalizi ya maonyesho hayo kufanya tathmini ya ubora wa bidhaa hizo kuona unakidhi mahitaji ya soko na watumiaji.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa amesisitiza wananchi kushiriki kikamilifu maadhimisho ya siku hiyo ya wakulima ili waweze kujipatia utaalamu mbalimbali wa kuendesha shughuli zinazohusu masuala ya kilimo, ufugaji na Uvuvi.
Maadhimisho hayo ya Kanda ya Mashariki yatahusisha mikoa ya Tanga, Pwani, Dar Es Salaam na Morogoro.
Pichani ni washiriki wa kikao hicho wakiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Katibu Tawala Wilaya ya Kibiti Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kibiti pamoja na wataalam wa Idara ya Kilimo, mifugo na Uvuvi Kibiti ambao pia walipata fursa ya kutembelea vipando vya Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti vilivyopo kwenye Uwanja huo.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.