Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo, ameagiza maonyesho ya biashara na uwekezaji ya Mkoa wa Pwani kuwa ya kitaifa kuanzia mwaka 2025, yakisimamiwa rasmi na Wizara ya Viwanda na Biashara.
Dk. Jafo alitoa agizo hilo leo disemba 17.2024, wakati akizindua maonyesho ya biashara yanayofanyika kwa mara ya nne mkoani humo, yakihusisha wawekezaji na wajasiriamali wadogo kutoka mkoa huo. Waziri huyo alisema kuwa maonyesho ya Mkoa wa Pwani yamekuwa yakifikia viwango vya kitaifa, na hivyo ni muhimu kuyaendeleza kwa ngazi hiyo ili kuvutia wawekezaji zaidi.
“Kuanzia mwaka 2025, maonyesho haya yawe ya kitaifa na yasimamiwe na Wizara ya Viwanda na Biashara kama yalivyo maonyesho mengine makubwa nchini. Hili ni agizo rasmi kwa Katibu Mkuu wa Wizara,” alisema Dk. Jafo.
Aidha, Waziri Jafo alizitaka taasisi wezeshi kuhakikisha haziwi kikwazo kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza nchini, akisisitiza umuhimu wa utoaji wa huduma bora ili kuvutia wawekezaji wapya.
Katika hatua nyingine, alihimiza wazalishaji wa bidhaa kuhakikisha wanazingatia ubora wa bidhaa zao ili ziweze kushindana kwenye masoko ya ndani na kimataifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, alitoa wito kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuhakikisha wanajenga bomba la gesi katika maeneo ya uwekezaji mkoani humo ili kurahisisha upatikanaji wa nishati ya gesi kwa viwanda.
Kunenge alisema maboresho makubwa kwenye sekta ya umeme yameongeza uzalishaji wa megawati kwa asilimia 19, hatua ambayo imerahisisha uzalishaji kwa wawekezaji wa viwanda. Hata hivyo, alisema baadhi ya wawekezaji wanahitaji nishati ya gesi kwa ajili ya uzalishaji.
Mkoa wa Pwani kwa sasa una viwanda 1,533, kati ya hivyo viwanda vikubwa ni 78. Mkoa huo pia unaendelea kuboresha miundombinu ya uwekezaji, huku maeneo makubwa zaidi yakitengwa kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vipya.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.